Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

DAS KARAGWE AAGIZA URATIBU WA PAMOJA KUIMARISHA USALAMA SEKTA YA USAFIRI MAJINI

Imewekwa: 14 April, 2026
DAS KARAGWE AAGIZA URATIBU WA PAMOJA KUIMARISHA USALAMA SEKTA YA USAFIRI MAJINI

Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Karagwe, Bw. Rasul Shandala, ameagiza taasisi za umma kushirikiana kwa karibu ili kuimarisha usalama na ufanisi katika sekta ya usafiri wa majini, hususan katika maeneo ya Ziwa Victoria na mipaka ya nchi jirani.

Ameyasema hayo leo, tarehe 10 Aprili, 2026 wakati akizungumza na maafisa kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), na Shirika la Bima la Taifa (NIC) walipotembelea ofisni za wilayani Karagwe. 

Bw. Shandala amesisitiza kuwa kuna umuhimu wa uratibu wa pamoja kati ya taasisi ikiwemo TASAC, NIC na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya kazikwakushirikiana ili kuhakikisha usimamizi madhubuti wa shughuli zote za usafiri wa majini ikiwa ni pamojana kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya usalama majini, pamoja na kuhamasisha wasafirishaji na abiria kuhusu umuhimu wa bima ili kujikinga na majanga yanayoweza kujitokeza. 

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha vyombo vyote vya usafiri wa majini vinasajiliwa na kufanyiwa ukaguzi wa mara kwa mara pamoja na kudhibiti mialo isiyo rasmi ili kuongeza mapato ya Serikali.

Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Kagera, Nahodha Mzee Mvihanga, amesema kuwa TASAC itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria na kanuni za usafiri wa majini, ikiwa ni pamoja na usajili wa vyombo vyote vinavyotoa huduma. 

Nahodha Mvihanga ameongeza kuwa ni muhimu manahodha wa vyombo kuwa na ujuzi na sifa stahiki za uendeshaji, huku akihimiza uboreshaji wa mazingira rafiki kwa wadau wa sekta hiyo ili kukuza uchumi wa maeneo husika.

Naye Afisa Bima wa Mkoa wa Kagera, Bw. Alfred Bwojo, amesema NIC kwa kushirikiana na TASAC itaendelea kutoa elimu ya bima kwa umma ili kuongeza uelewa wa faida zake, sambamba na kupanua wigo wa huduma za bima nchini.

Bw. Bwojo ameongeza kuwa juhudi hizo zinalenga kuongeza ushirikishwaji wa kifedha na kuwafanya wananchi wengi zaidi kunufaika na huduma za bima.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo