BOTI MBILI ZA UTAFUTAJI NA UOKOAJI (SARs) KATIKA ZIWA VICTORIA ZAWASILI NCHINI

Boti mbili (2) za utafutaji na uokoaji ambazo ni sehemu ya Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria (MLVMCTP) zimewasili katika Bandari ya Dar es Salaam kutoka Uturuki zilipokua zinatengenezwa na Mkandarasi Loça Mühendislik.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 18 Julai, 2025 katika Bandari ya Dar es salaam wakati wa kushuhudia kuwasili kwake, Mha. Saidi Kaheneko, Kaimu Meneja wa Usajili na Ukaguzi wa Vyombo vya Usafiri Majini amesema kuwa ujio wa boti hizo ni hatua kubwa katika kuimarisha usalama wa usafiri wa majini katika Ziwa Victoria.
"Boti hizi zina uwezo wa kasi kubwa na zitatumika katika kusaidia kazi za utafutaji na uokoaji wa haraka kwa waathirika wa ajali za majini, hali itakayopunguza madhara yatokanayo na dharura katika Ziwa Victoria," amesema Mha, Kaheneko.
Boti hizo zinatarajiwa kusafirishwa kwenda mkoani Mwanza kwa ajili ya kusaidia katika operesheni ya utafutaji na uokoaji Ziwa Victoria.
Serikali kupitia TASAC imeendelea kuboresha usalama wa usafiri wa majini, ili kupunguza ajali, na kukuza biashara na usafiri usio na mashaka nchini.