Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

BODI YA WAKURUGENZI TASAC YAVUTIWA NA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA UCHUKUZI  MKOANI KAGERA

Imewekwa: 28 April, 2025
BODI YA WAKURUGENZI TASAC YAVUTIWA NA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA UCHUKUZI  MKOANI KAGERA

Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imeeleza kuvutiwa na uwekezaji unaofanywa na Serikali na sekta binafsi mkoani Kagera.

Hayo yamesemwa leo tarehe 25 Aprili,2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC, Nahodha Mussa Mandia alipokuwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa  wa Kagera.  Naho.  Mandia, akiwa na wajumbe wa Bodi, alifika ofisini hapo kuelezea lengo la ziara ya Bodi inayofanyika mkoani humo. 

Aidha, Nah.  Mandia ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na TASAC katika kusimamia  usafiri salama majini.

"Serikali yetu ni sikivu na tumeona inavyotatua changamoto za usafiri majini na kuwaletea wananchi maendeleo. Tumeona bandari zinajengwa mialo rasmi imeanzishwa na sekta binafsi imewekeza katika viwanda vya kuchakata minofu ya samaki vimejengwa kutoka kiwanda kimoja hadi vitatu. Hii imeleta manufaa ya ajira kwa wananchi wa maeneo haya na Tanzania kwa ujumla. Naomba shukrani zimfikie Mkuu wa Mkoa, Fatuma Mwassa," amesema Naho. Mandia.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe.Erasto Sima, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Kagera, amesema kuwa ujio wa Bodi ya TASAC utasaidia katika kukusanya kero za  wananchi na kuzishughulikia kwa kushirikisha wadau.

" Ujio wenu ni muhimu na utatusaidia kutatua kero za wananchi. Tunamshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu kwa kujenga miundombinu ambayo itasaidia kuchagiza ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Kagera,” amesema Mhe. Sima.

Mhe. Sima ameongeza kuwa Serikali ya  Mkoa itaendelea kushirikiana na TASAC katika kuhakikisha usalama na ulinzi wa usafiri majini unaimarishwa mkoani humo, na kuiomba TASAC kuongeza idadi ya wafanyakazi mkoani Kagera.

Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC ipo mkoani Kagera kwa ziara ya siku sita kwa ajili ya kutembelea maeneo ya bandari, mialo, maziwa madogo na wathibitishaji wa uzito wa mizigo ikiwemo makasha ya samaki yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo