BALOZI WA TANZANIA NCHINI UINGEREZA AHUTUBIA MKUTANO MKUU WA SHIRIKA LA BAHARI DUNIANI
Mhe. Mbelwa Kairuki, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uingereza, ametoa wito kwa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) kuongeza ushirikishwaji wa nchi zinazoendelea katika mageuzi ya kijani ya sekta ya usafiri wa majini.
Akizungumza katika Mkutano wa 34 wa Baraza Kuu la IMO unaofanyika London, Balozi Kairuki aliielezea Tanzania kama “lango la bahari” kwa mataifa sita yasiyo na bandari kavu. Alifafanua kuwa nchi imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Bandari ya Dar es Salaam kupitia miradi ya upanuzi wa gati, maboresho ya ufanisi wa upakiaji na upakuaji mizigo, na uboreshaji wa miundombinu ya reli na barabara ili kuendana na ongezeko la biashara ya kikanda.
Akiizungumzia ajenda ya usalama, Balozi Kairuki alisema Tanzania inaendelea kuipa kipaumbele usalama wa baharini kupitia utekelezaji kamili wa Kanuni za ISPS katika bandari zote, kuimarisha ukaguzi wa meli, pamoja na ushiriki katika Mkataba wa Djibouti kwa ajili ya kukabiliana na uharamia na uhalifu wa baharini.
Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, aliweka bayana kuwa Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kuridhia Kiambatisho cha VI cha Mkataba wa MARPOL, na inaunga mkono malengo ya kimataifa ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafu kutoka kwenye sekta ya usafiri wa majini. Hata hivyo, alisisitiza kuwa utekelezaji wa malengo hayo unahitaji kuzingatia usawa kwa kuongeza fedha za tabianchi, uhamishaji wa teknolojia na uwekezaji katika miundombinu ya bandari za kijani ili kusaidia nchi zinazoendelea kutekeleza majukumu hayo.
Akihitimisha, Balozi Kairuki alisisitiza dhamira ya Tanzania kuendelea kutekeleza wajibu wake ndani ya IMO, kuimarisha ushirikiano wa kikanda, na kushirikiana na nchi wanachama katika kujenga sekta ya baharini iliyo salama zaidi, safi zaidi na jumuishi kwa manufaa ya wote.