TAARIFA KWA UMMA SENSA YA VYOMBO VIDOGO VYA USAFIRI WA MAJINI NA UVUVI TANZANIA BARA MWAKA 2021

Imewekwa: Oct 05, 2021


TAARIFA KWA UMMA

SENSA YA VYOMBO VIDOGO VYA USAFIRI WA MAJINI NA UVUVI TANZANIA BARA MWAKA 2021

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wanatoa taarifa kwa umma kuwa, watafanya Sensa ya vyombo vidogo vya usafiri wa majini, ikiwa ni pamoja na vyombo vya uvuvi Tanzania Bara kuanzia tarehe 1 hadi 30 Oktoba 2021. Sensa hiyo itafanyika katika maeneo yote yenye vyombo vidogo vya usafiri wa majini na vile vya uvuvi katika mikoa yote ya mwambao wa Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na maeneo mengine ya maji yanayotumika katika usafiri wa majini na uvuvi (mito na mabwawa) yaliyoko mikoa yote ya Tanzania Bara.

Malengo makuu ya Sensa hiyo ni kuorodhesha vyombo vyote vidogo vya usafiri majini na uvuvi ili kuandaa kanzi data (database) ya vyombo hivyo. Kanzi data hiyo itatumika katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi, pamoja na utekelezaji wa sera na sheria za usalama majini.

TASAC inatoa wito kwa wasafirishaji, waendeshaji na wamiliki wa vyombo vidogo katika bahari, maziwa, mito na mabwawa kujitokeza na kutoa ushirikiano kwa wadadisi watakaopita katika maeneo yao ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi.

Hakuna gharama yoyote itakayotozwa kuhusiana na zoezi la Sensa ya vyombo vidogo vya usafiri majini na uvuvi.

Imetolewa na:

MKURUGENZI MKUU

SHIRIKA LA UWAKALA WA MELI TANZANIA (TASAC)