TAARIFA KWA UMMA: MKAKATI WA KUJIKINGA NA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA KORONA KWA WATOA HUDUMA KATIKA SEKTA YA USAFIRI NA USAFIRISHAJI MAJINI.

Imewekwa: Jul 24, 2021


Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania linawaagiza watoa huduma wote katika sekta ya usafiri na usafirishaji majini kuweka mikakati ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Korona.

Watoa huduma wote ikiwa ni pamoja na wamiliki wa vyombo vya usafiri na usafirishaji majini, watoa huduma za bandari, uwakala wa meli na waondoshaji wa shehena katika bandari wanaagizwa kutekeleza yafuatayo:

  1. Wamiliki wa vyombo vya usafirishaji majini wanyunyizie dawa za kuua virusi katika vyombo vyao kila mwisho wa safari.
  2. Wahudumu na abiria wote wanaoingia na wanaotoka katika vyombo vya usafiri majini ikiwa ni pamoja na meli, mitumbwi na vivuko wanawe mikono kwa maji tiririka na sabuni.
  3. Kuzingatia idadi ya abiria wanaoruhusiwa kwenye vyombo wanaposafiri kutoka eneo moja kwenda eneo jingine ili kuepusha msongamano.
  4. Kuweka vyombo vya kunawia mikono katika ofisi za watoa huduma za bandari, uwakala wa meli, wahakiki na waondoshaji wa shehena bandari nchini.
  5. Kuhakikisha tahadhari ya kujikinga na virusi vya Korona inatolewa ndani ya vyombo vya usafiri kwa kutumia redio na runinga zilizopo kwenye vyombo hivyo.

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania litasimamia utekelezaji wa maagizo haya kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya udhibiti wa huduma za Bandari na usafiri majini, ulinzi na usalama wa usafiri majini.

Imetolewa na:

Mkurugenzi Mkuu,

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania - TASAC,

24 Julai, 2021