WAZIRI MKUU DKT. MWIGULU NCHEMBA AFUNGUA RASMI MAONESHO YA NANENANE 2026
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewahimiza washiriki wa Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Nanenane 2026 kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vinavyokubalika wakati wote ili kukidhi mahitaji ya masoko ya ndani na kimataifa.
Dkt. Nchemba amesema uzalishaji wa bidhaa bora utaiwezesha Tanzania kushindana katika masoko ya dunia, kukuza biashara na kuongeza kipato cha wananchi.
Amesisitiza kuwa ubora wa bidhaa na huduma zinazotolewa katika Maonesho ya Nanenane unapaswa kuwa endelevu na usiishie wakati wa maonesho pekee. Hivyo, wazalishaji wanapaswa kuhakikisha bidhaa zinazowafikia walaji zinaendelea kuwa na ubora unaolingana na zile wanazozionesha wakati wa maonesho.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo tarehe 1 Agosti, 2026, alipofungua rasmi Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yenye Kauli mbiu “Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050” yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika maonesho hayo, likitoa elimu kuhusu majukumu yake ya kusimamia usafiri salama na endelevu majini, udhibiti wa sekta ya usafiri wa majini pamoja na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.
Kupitia maonesho hayo, TASAC pia inaelimisha wananchi kuhusu usalama wa vyombo vya majini, umuhimu wa kutumia vyombo vilivyosajiliwa na kukaguliwa, kuvaa vifaa vya kujiokolea na kuzingatia masharti ya usalama wakati wa safari.
Maonesho hayo yaliyofunguliwa rasmi leo tarehe 1 Agosti, 2026 yanayotarajiwa kufikia kilele chake tarehe 8 Agosti, 2026 yanawakutanisha wakulima, wafugaji, wavuvi, watafiti, wawekezaji, taasisi za Serikali na sekta binafsi kwa lengo la kuonesha teknolojia za kisasa, kubadilishana maarifa na kujenga fursa za biashara.