Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TAHADHARI YA EL NINO: TASAC YATOA ELIMU YA USALAMA KWA WADAU WA USAFIRI MAJINI NGARA

Imewekwa: 17 September, 2026
TAHADHARI YA EL NINO: TASAC YATOA ELIMU YA USALAMA KWA WADAU WA USAFIRI MAJINI NGARA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limewataka wananchi wanaojihusisha na usafiri na shughuli nyingine za majini wilayani Ngara, mkoani Kagera, kuchukua tahadhari kutokana na uwezekano wa mvua za El Niño, huku wakisisitizwa kufuatilia kwa karibu taarifa rasmi za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

TASAC imetoa wito huo wakati wa zoezi la utoaji elimu kwa wananchi katika kivuko cha MV Ruvuvu, kilichopo Kata ya Rusumo wilayani Ngara, ambapo waendeshaji na watumiaji wa vyombo vya usafiri majini walipatiwa elimu kuhusu hatua za kuchukua ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Kagera, Nahodha Mzee Ally Mvihanga amesisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari mapema na kuzingatia taarifa za hali ya hewa, hususan pale zinapotolewa tahadhari kuhusu mabadiliko makubwa ya hali ya hewa.

Wamesema wananchi wanapaswa kuepuka safari zisizo za lazima wakati hali ya hewa inapokuwa hatarishi, pamoja na kuhakikisha kuwa safari za majini zinafanyika kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya usalama.

Aidha, Nahodha Mvihanga amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha vyombo vya usafiri majini vina vifaa muhimu vya usalama na uokoaji, ikiwemo vifaa vya kujiokoa, pamoja na kutoa taarifa mapema kwa mamlaka husika endapo kutatokea hali inayoweza kuhatarisha usalama wa watu, vyombo au mali.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi walioshiriki katika zoezi hilo, akiwemo Justine Jacob na Nahodha Odeth Aporinary, wamesema elimu iliyotolewa na TASAC imewaongezea uelewa kuhusu umuhimu wa kuchukua tahadhari wakati wa kufanya shughuli za majini katika kipindi ambacho kuna uwezekano wa mabadiliko ya hali ya hewa.

Wameahidi kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na TASAC na kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa kutoka TMA, huku wakisisitiza umuhimu wa kuweka usalama wa abiria, waendeshaji na mali kuwa kipaumbele wakati wote wa shughuli za usafiri majini.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo