Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

WAZIRI MKUU DKT. MWIGULU NCHEMBA AFUNGA RASMI MAONESHO YA TISA YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA

Imewekwa: 03 October, 2026
WAZIRI MKUU DKT. MWIGULU NCHEMBA AFUNGA RASMI MAONESHO YA TISA YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesisitiza umuhimu wa kuendeleza sekta ya madini kwa kuzingatia ushiriki wa Watanzania, kuongeza thamani ya madini hapa nchini na kuhakikisha rasilimali hizo zinatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Ameyasema hayo leo tarehe 03 Oktoba, 2026 wakati akifunga rasmi Maonesho ya Tisa (9) ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika mkoani Geita, ambapo amewataka wadau wa sekta hiyo kutumia ipasavyo fursa zinazotokana na uwepo wa rasilimali za madini kwa kuongeza tija, uzalishaji na thamani ya madini.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia uhifadhi wa mazingira, usalama kazini na maslahi ya jamii zinazozunguka maeneo ya uchimbaji madini.

Maonesho hayo yametoa fursa kwa wachimbaji wadogo na wakubwa, wafanyabiashara, wataalamu, taasisi za Serikali, wawekezaji na wadau wengine kuonesha bidhaa, huduma, teknolojia na ubunifu katika sekta ya madini, pamoja na kuwawezesha wananchi kupata elimu kuhusu taratibu, fursa na masoko ya madini.

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ni miongoni mwa taasisi zilizoshiriki katika maonesho hayo, likitoa elimu kuhusu jukumu la kipekee la Ugomboaji na Uondoshaji wa shehena zinazoingizwa au kutoka nchini kwa bidhaa bidhaa mahususi zenye maslahi mapana kwa nchi na taifa kwa ujumla ambazo ni Silaha na vilipuzi, Makinikia, Kemikali zinazotumika kwenye kampuni za uchimbaji madini, Nyara za Serikali na Wanyama hai kama walivyoainishwa katika Sheria ya Uhifadhi wa wanyama pori.

Maonesho hayo yenye kaulimbiu “Madini ni Utajiri, Tuwajibike kwa Pamoja Kufika Dira ya Taifa 2050”  yamefanyika kuanzia Septemba 23 hadi Oktoba 3, 2026, yakishirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, wakiwemo wachimbaji, wawekezaji, wajasiriamali, taasisi za Serikali, taasisi za fedha pamoja na wazalishaji na wauzaji wa teknolojia na vifaa vya uchimbaji.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo