Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAWATAKA WAHITIMU CHAMAZI KUCHANGAMKIA FURSA ZA SEKTA YA USAFIRI MAJINI

Imewekwa: 03 October, 2026
TASAC YAWATAKA WAHITIMU CHAMAZI KUCHANGAMKIA FURSA ZA SEKTA YA USAFIRI MAJINI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limewataka wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Chamazi kuchangamkia fursa zinazopatikana katika tasnia ya ubaharia na sekta ya usafiri kwa njia ya maji, ikiwemo taaluma za uhandisi wa meli, bandari, ugomboaji wa shehena, sheria za bahari, mazingira na TEHAMA.

Wito huo umetolewa na Bi. Pili Mazowea, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, wakati wa Mahafali ya 18 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Chamazi yaliyofanyika Oktoba 1, 2026, sambamba na maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo.

Akizungumza katika mahafali hayo, Bi. Mazowea aliwapongeza wahitimu kwa kukamilisha hatua hiyo ya elimu, huku akisisitiza kuwa mahafali si mwisho wa safari yao, bali ni mwanzo wa hatua mpya yenye fursa, changamoto na majukumu mbalimbali.

Aliwahimiza wahitimu kuendelea na elimu, kujenga nidhamu, uadilifu, bidii, ubunifu, ujuzi na uwajibikaji, pamoja na kuwa na dhamira ya kulitumikia Taifa.

Aidha, alieleza kuwa TASAC ina jukumu la kusimamia na kudhibiti shughuli mbalimbali za sekta ya usafiri majini, ikiwemo usalama na ulinzi wa usafiri majini, udhibiti wa huduma za usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji, pamoja na kulinda mazingira ya bahari na maeneo yanayohusiana na shughuli za usafiri majini.

Bi. Mazowea alisisitiza kuwa sekta ya usafiri majini haihitaji manahodha pekee, bali inahitaji wataalamu wa fani mbalimbali wakiwemo wahandisi wa meli, wataalamu wa bandari na lojistiki, wanasheria wa baharini, wataalamu wa mazingira, TEHAMA, biashara, uchumi na fedha.

Aliongeza kuwa fursa zipo na kuwataka wahitimu kujiandaa kielimu na kitaaluma ili waweze kushiriki katika maendeleo ya sekta ya usafiri majini na Taifa kwa ujumla.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo