WAZIRI MKUU AFUNGUA MKUTANO WA 10 WA MOESNA, AITAKA AFRIKA KUIMARISHA MIFUMO YA USAFIRISHAJI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka nchi za Afrika kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya uchukuzi ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, kukuza biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Dkt. Nchemba ametoa wito huo leo, Oktoba 15, 2026, wakati akifungua Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri la Nchi Wanachama wa Shirika la Wanamaji la Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini (MOESNA), uliofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam.
Amesema kuunganisha usafiri wa majini na barabara pamoja na reli kutapunguza muda na gharama za usafirishaji, huku kukirahisisha upatikanaji wa masoko kwa nchi za Afrika.
Ameeleza kuwa ukosefu wa miundombinu inayounganisha nchi hizo unasababisha mizigo inayosafirishwa ndani ya bara hilo kuchukua muda mrefu kufika inakokwenda.
Akitoa mfano, amesema usafirishaji wa maziwa kutoka Uganda kwenda Afrika Magharibi ulichukua takribani miezi miwili na nusu hadi karibu miezi mitatu, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuboresha mifumo ya usafirishaji wa kikanda.
Dkt. Nchemba amesisitiza kuwa miundombinu imara ni msingi wa kuunganisha uchumi wa Afrika na kuongeza ushindani wa bidhaa zake katika masoko.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, amesema maendeleo ya sekta ya uchukuzi ni msingi muhimu wa kukuza biashara, kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa nchi za ukanda huo.
Prof. Mbarawa amesema katika kipindi cha uenyekiti, msukumo umewekwa katika kuimarisha usafirishaji wa mizigo, kuongeza ushiriki wa nchi za Afrika katika umiliki na uendeshaji wa meli, pamoja na kuendeleza wataalamu na kukuza ujuzi katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji.
Mawaziri hao wamejadili mikakati ya kuimarisha uunganishaji wa nchi hizo, kurahisisha biashara, kuboresha huduma za bandari na usafirishaji wa mizigo, pamoja na kukuza ushirikiano katika sekta ya uchukuzi.
Katika mkutano huo, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) linashiriki katika kujadili mikakati ya kuendeleza sekta ya uchukuzi wa majini, kuimarisha usalama wa usafiri na kuboresha ufanisi wa huduma za usafirishaji.