MAKAMU WA RAIS AWATAKA WATANZANIA KURITHI MISINGI YA BABA WA TAIFA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka Watanzania kuendeleza urithi na misingi ya uongozi iliyoachwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa vitendo, hususan katika kulinda amani, umoja na mshikamano wa Taifa.
Mhe. Ndejembi ameyasema hayo alipowahutubia maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Rukwa katika sherehe za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2026, zilizofanyika katika Uwanja wa CCM Nelson Mandela, Manispaa ya Sumbawanga.
Sherehe hizo zimefanyika sambamba na kumbukizi ya miaka 27 tangu kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999, pamoja na Wiki ya Vijana.
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais amewataka Watanzania kutafakari mchango wa Mwalimu Nyerere katika kupigania uhuru, kujenga Taifa na kusimamia misingi ya Ujamaa na Kujitegemea.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendeleza falsafa za Mwalimu Nyerere kwa vitendo kupitia uwekezaji katika elimu bila malipo, afya, maji na kilimo, kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, amesema Mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka 2026 zimekagua na kuzindua miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 2.24 nchini kote, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mapema, Makamu wa Rais alishiriki Misa Takatifu ya kumuombea Baba wa Taifa iliyofanyika katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Epifania, Jimbo Katoliki la Sumbawanga.
Misa hiyo iliongozwa na Askofu Mstaafu Damian Kyaruzi na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba; mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere; Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Makongoro Nyerere; pamoja na viongozi wengine wa Chama na Serikali.