Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

WAZIRI MKUU AELEKEZA KUIMARISHWA KWA USALAMA MAJINI ZIWA VICTORIA

Imewekwa: 22 May, 2026
WAZIRI MKUU AELEKEZA KUIMARISHWA KWA USALAMA MAJINI ZIWA VICTORIA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka mamlaka zinazohusika na usalama majini nchini kuendelea kuimarisha mifumo ya uokoaji pamoja na vifaa vya usalama ili kupunguza ajali zinazotokea katika shughuli za usafiri na uvuvi ndani ya Ziwa Victoria.

Waziri Mkuu amesema hayo leo tarehe 21 Mei 2026 wakati akiongoza kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria yaliyofanyika jijini Mwanza.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Dkt. Nchemba pia alisisitiza umuhimu wa kulinda na kuhifadhi rasilimali za Ziwa Victoria kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, huku akitoa rai kwa serikali na wananchi wa nchi zote za ukanda wa ziwa hilo kushirikiana katika kupambana na uchafuzi wa mazingira, uvuvi haramu pamoja na shughuli nyingine zinazohatarisha uhai wa ziwa hilo.

Aidha, Waziri Mkuu alihimiza matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa shughuli za ziwa ikiwemo ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi, usafiri majini na hali ya mazingira ili kuongeza ufanisi wa usimamizi na upangaji wa mipango ya maendeleo.

Maadhimisho hayo yaliwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri majini, uvuvi, mazingira pamoja na taasisi za serikali, ambapo Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) lilishiriki katika maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria yaliyoanza rasmi tarehe 18 Mei 2026 na kufungwa leo tarehe 21 Mei 2026 jijini Mwanza.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo