WATUMISHI WA TASAC WASISITIZWA KUZINGATIA MAADILI NA WELEDI KAZINI
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, amefungua rasmi mafunzo ya awali kwa jumla ya watumishi 55, kati yao wapya wakiwa 13 pamoja na waliohamia TASAC wakiwa 42 kwa kusisitiza kuzingatia nidhamu, uwajibikaji na uadilifu katika utumishi wa umma.
Akizungumza leo tarehe 27 Agosti, 2026, katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa PSSSF Garden Avenue jijini Dar es Salaam, Bw. Salum amesisitiza kuwa watumishi wapya wanapaswa kuwa na maadili ya Utumishi wa Umma, kujifunza kwa bidii ili kuwa weledi na wabobezi katika sekta ya usafiri majini na kufanya kazi kwa ufanisi, kwa kuwa TASAC ni taasisi yenye jukumu la udhibiti.
“Mafunzo haya yanawawezesha kuwa watumishi bora, wenye maadili thabiti na weledi katika majukumu yenu. Pia yanajenga taswira chanya kwa umma na kuifanya TASAC kuaminika zaidi katika utekelezaji wa majukumu yenu”, amesema Bwn. Salum
Mafunzo hayo ya siku 8 yaliyoanza tarehe 26 Agosti,2026 na yanatariwa kuhitimishwa tarehe 4 Septemba,2026 yamejikita katika kuwajengea washiriki uelewa wa maadili ya utumishi wa umma, haki na wajibu wao, Majukumu ya TASAC pamoja na Sheria zinazowaongoza. Pia yatasaidia kuwajenga na kuwa watumishi wema wenye ushirikiano na watumishi waliowakuta kazini, kuyajua mazingira ya kazini ili kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania.
Mojawapo ya mada zinazofundishwa ni pamoja Maadili ya Utumishi wa Umma, Uendeshaji wa Utumishi wa Umma, Utunzaji wa Kumbukumbu, kanuni za kudumu za utumishi wa Umma, Dhana utoaji Huduma bora kwa Mteja na Muundo Serikali katika kuendesha Shughuli zake. TASAC inatoa Mafunzo hayo ikilenga kuwafanya kuwa watumishi bora, wema, wenye nidhamu na weledi ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.