Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

RC TANGA: WANANCHI JITOKEZENI KUSHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA USAFIRI MAJINI DUNIANI

Imewekwa: 19 September, 2026
RC TANGA: WANANCHI JITOKEZENI KUSHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA USAFIRI MAJINI DUNIANI

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, amewataka wananchi wa Mkoa wa Tanga na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki Maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani (World Maritime Day 2026), yatakayofanyika mkoani Tanga kuanzia Septemba 21 hadi 24, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari, leo Septemba 18, 2026, Mhe. Balozi Dkt. Batilda amesema maadhimisho hayo yataongozwa na kaulimbiu “From Policy to Practice: Powering Maritime Excellence”, inayosisitiza utekelezaji wa sera, sheria, mikakati na miongozo katika kuimarisha usalama wa usafiri majini, ustawi wa mabaharia na maendeleo ya sekta ya bahari.

Amesema shughuli zitakazofanyika katika kipindi hicho ni pamoja na utoaji wa elimu kuhusu usalama wa usafiri majini, maonesho ya huduma zinazotolewa na taasisi za Serikali na wadau, kampeni za matumizi salama ya vyombo vya majini, elimu kwa wanafunzi kuhusu fursa za sekta ya bahari, warsha, shughuli za kijamii, uchangiaji damu pamoja na zoezi la uokozi wakati wa dharura.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, uzinduzi rasmi utafanyika Septemba 21, 2026 katika Viwanja vya Kijiji cha 21, huku kilele cha maadhimisho hayo kikifanyika katika eneo hilo Septemba 24, 2026.

Aidha, amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu na huduma za usafiri majini, ikiwemo Bandari ya Tanga, iliyofanyiwa maboresho kwa uwekezaji wa Sh bilioni 429.1.

Amesema uwekezaji huo umeongeza ufanisi wa bandari hiyo, ambapo meli zinazohudumiwa zimeongezeka kutoka 118 mwaka 2019/20 hadi 458 mwaka 2024/25, huku shehena ikiongezeka kutoka tani 470,611 hadi tani 1,326,415.

Mhe. Balozi Dkt. Batilda amewapongeza mabaharia wa Tanzania kwa mchango wao katika usafirishaji wa watu na mizigo, na kuwataka wadau kushirikiana na Serikali kuimarisha usalama wa usafiri majini, kulinda mazingira na kuboresha huduma.

Ameongeza kuwa maadhimisho hayo ni fursa kwa wananchi kujifunza kuhusu sekta ya bahari, kutambua fursa za ajira na uwekezaji, na kushiriki katika juhudi za kuimarisha uchumi wa buluu nchini.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo