TAHADHARI YA EL NIÑO: TASAC YAWATAKA WADAU KARAGWE NA MISSENYI KUFUATA SHERIA
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limewataka wananchi, wamiliki, waendeshaji, manahodha na watumiaji wa vyombo vya usafiri majini katika Wilaya za Karagwe na Missenyi, mkoani Kagera, kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama wa usafiri majini, hususan katika kipindi hiki cha utabiri wa mvua za Vuli zinazoweza kuathiriwa na El Niño.
TASAC imetoa wito huo wakati ikiendelea kutoa elimu na uhamasishaji kwa wadau wa mialo ya Ruwazi na Kabindi kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa kutokana na uwezekano wa mvua kubwa, upepo mkali, mafuriko na mabadiliko ya hali ya maji yanayoweza kuongeza hatari katika shughuli za usafiri majini.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Kagera, Nahodha Mzee Mvihanga, akiwa ameambatana na Meneja Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa TASAC, Bw. Saidi Mkabakuli, amewataka wamiliki na waendeshaji wa vyombo kuhakikisha safari zinafanyika kwa kuzingatia matakwa ya kisheria na kiusalama.
Amesisitiza umuhimu wa vyombo kufanyiwa ukaguzi unaohitajika, kutopakia abiria au mizigo kupita uwezo uliowekwa, pamoja na kuhakikisha vifaa vya usalama, ikiwemo jaketi za kujiokoa (life jackets), vinapatikana na kutumiwa ipasavyo.
Aidha, Nahodha Mvihanga amewataka wadau kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kabla na wakati wa safari, na kuchukua hatua stahiki pale tahadhari zinapotolewa.
Kwa upande wake, Bw. Saidi Mkabakuli amesema TASAC itaendelea kutoa elimu kwa wadau katika maeneo mbalimbali ili kuongeza uelewa kuhusu usalama wa usafiri majini na namna ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa.
Baadhi ya wananchi na wasafiri waliopata elimu hiyo wameipokea kwa mtazamo chanya, wakisema imewasaidia kuelewa umuhimu wa kufuata sheria, kutumia vifaa vya usalama na kuzingatia taarifa za hali ya hewa wakati wa kupanga safari.
TASAC imeendelea kusisitiza kuwa usalama wa usafiri majini ni jukumu la pamoja na kila mdau anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria na maelekezo ya mamlaka husika.