WADAU WAENDELEA KUTEMBELEA BANDA LA TASAC NA KUPATA ELIMU KATIKA MAONESHO YA MEATF
Wananchi na wadau mbalimbali wanaendelea kutembelea Banda la Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) katika Maonesho ya 20 ya Biashara ya Afrika Mashariki (Mwanza East Africa Trade Fair – MEATF), yanayofanyika jijini Mwanza kuanzia tarehe 28 Agosti hadi 6 Septemba 2026.
Wakiwa Bandani hapo wananchi wanapatiwa elimu ya masuala mbalimbali kuhusu usalama wa vyombo vya majini, udhibiti wa huduma za usafiri wa majini, shughuli za uwakala wa meli pamoja na utunzaji wa mazingira katika maeneo ya majini. Aidha, wataalamu wa TASAC wanaendelea kujibu maswali na kutoa ufafanuzi kuhusu huduma zinazotolewa na Shirika.
Ushiriki wa TASAC katika MEATF unaendelea kuwa sehemu muhimu ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu usafiri salama na wenye ufanisi wa majini. Kupitia mazungumzo ya moja kwa moja na wataalamu wa TASAC, wananchi na wadau wanapata nafasi ya kutoa maoni, kuuliza maswali na kueleza changamoto wanazokutana nazo katika shughuli zao zinazohusiana na sekta ya usafiri wa majini.
TASAC inaendelea kuwasisitiza wananchi na wadau mbalimbali kutumia fursa ya Maonesho ya MEATF kutembelea banda lake na kupata elimu kuhusu huduma na majukumu ya Shirika, huku wakizingatia umuhimu wa usalama, ufanisi na utunzaji wa mazingira katika shughuli za usafiri wa majini.
Maonesho hayo yanafanyika chini ya Kaulimbiu: “Usalama & Amani ni Kichocheo cha Biashara na Uwekezaji Hapa Nchini.”