Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

MAADHIMISHO YA SIKU YA USAFIRI KWA NJIA YA MAJINI DUNIANI YAFUNGULIWA RASMI JIJINI TANGA

Imewekwa: 22 September, 2026
MAADHIMISHO YA SIKU YA USAFIRI KWA NJIA YA MAJINI DUNIANI YAFUNGULIWA RASMI JIJINI TANGA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mha. Ali Said Bakar, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa SMZ, leo tarehe 21 Septemba 2026 amefungua rasmi Maadhimisho ya Siku ya Usafiri Majini Duniani 2026 katika Viwanja vya Kijiji cha 21, jijini Tanga.

Maadhimisho hayo yanafanyika kuanzia tarehe 21 hadi 24 Septemba 2026, yakiwa na kaulimbiu isemayo “From Policy to Practice: Powering Maritime Excellence”, inayotafsiriwa kwa Kiswahili “Kutoka Sera hadi Utekelezaji: Kuimarisha Ubora Katika Sekta ya Usafiri Majini.”

Akizungumza katika ufunguzi huo, Mha. Ali amesema kaulimbiu hiyo inasisitiza umuhimu wa kuhakikisha sera, sheria, kanuni na mikakati inayowekwa katika sekta ya usafiri majini inatekelezwa kwa vitendo na kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi na katika maendeleo ya sekta hiyo.

Amesema utekelezaji huo unapaswa kuonekana katika kuimarika kwa usalama wa vyombo vya usafiri majini, kupungua kwa ajali, kulindwa kwa mazingira ya bahari na vyanzo vya maji, kuongezeka kwa ufanisi wa bandari, matumizi ya teknolojia na upatikanaji wa wataalamu wenye ujuzi unaokidhi viwango vya kikanda na kimataifa.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa teknolojia katika kuboresha huduma, akieleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya kidijitali, ili kupunguza urasimu, kuongeza uwazi na kuharakisha utoaji wa huduma zinazohusiana na meli na shughuli za bandarini.

Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Wakili Judith Kakongwe, amewashukuru wadau kwa kudhamini na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo, akisema ushirikiano wao umechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha maadhimisho hayo.

Maadhimisho hayo yanawakutanisha viongozi, taasisi za Serikali, wamiliki na waendeshaji wa meli, mabaharia, taasisi za elimu na mafunzo pamoja na wadau wengine kujadili maendeleo, changamoto na mustakabali wa sekta ya usafiri majini.

Maadhimisho hayo yanaendelea mkoani Tanga hadi tarehe 24 Septemba 2026, yakilenga kuhamasisha utekelezaji wa sera kwa vitendo na kujenga sekta ya usafiri majini iliyo salama, yenye ufanisi na endelevu.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo