Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAIBUKA KINARA WA UTENDAJI BORA MIONGONI MWA MAMLAKA ZA UDHIBITI

Imewekwa: 19 November, 2026
TASAC YAIBUKA KINARA WA UTENDAJI BORA MIONGONI MWA MAMLAKA ZA UDHIBITI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeibuka mshindi wa kwanza katika tathmini ya utendaji kazi wa mikataba kati ya Katibu Mkuu na Wakurugenzi Wakuu wa Mamlaka za Udhibiti zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi, na kutunukiwa ngao maalumu ya kutambua utendaji bora.

Tuzo hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb.), kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, wakati wa kufunga Mkutano wa 19 wa Wadau wa Sekta ya Uchukuzi na Tathmini ya Utendaji Kazi uliofanyika katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza, Novemba 17, 2026.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Dkt. Mkama amesema tuzo hiyo ni uthibitisho wa juhudi zinazofanywa na mamlaka hizo katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kutoa huduma bora kwa wananchi na kuchangia maendeleo ya sekta ya uchukuzi.

Aidha, ameitaka TASAC kutumia mafanikio hayo kama chachu ya kuendelea kuimarisha utendaji wake, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika upangaji jumuishi, usalama wa huduma za uchukuzi, muunganiko wa kikanda na biashara ili kukuza maendeleo ya sekta hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mkurugenzi wa Huduma za Shirika, Bw. Hamid Mbegu, ameishukuru Wizara ya Uchukuzi kwa kutambua na kuthamini utendaji bora wa Shirika, akieleza kuwa tuzo hiyo ni motisha ya kuendelea kuboresha huduma na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Aidha, ameeleza kuwa TASAC inaendelea na maandalizi ya mageuzi ya kimuundo yanayolenga kulibadilisha Shirika kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Majini Tanzania, hatua itakayoliwezesha kujikita zaidi katika usimamizi na udhibiti wa shughuli za usafiri majini.

Amesema mageuzi hayo yanalenga kuimarisha usalama wa vyombo vya majini, usimamizi wa huduma za bandari na usafiri majini pamoja na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ufanisi wa udhibiti, kuboresha huduma na kuchochea ukuaji wa biashara ya ndani na kimataifa.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo