TASAC YATAKA WELEDI, UADILIFU KUIMARISHWA SEKTA YA FORODHA NA UGOMBOAJI
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa wito kwa wadau wa sekta ya forodha na ugomboaji kuendelea kuimarisha weledi, uadilifu na uzingatiaji wa sheria na taratibu ili kuongeza ufanisi wa huduma na kujenga mazingira bora ya biashara nchini.
Wito huo umetolewa na mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Sylvester Kanyika, wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TACAS) 2026, uliofanyika Leo tarehe 29 Septemba, 2026 katika Hoteli ya Holiday Inn, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo, Bw. Kanyika amesema TASAC na TACAS, licha ya kuwa na majukumu tofauti, zinaunganishwa na lengo la kuhakikisha shughuli za usafirishaji na uondoshaji wa mizigo zinafanyika kwa ufanisi, uwazi, usalama na kwa kuzingatia sheria.
Amesema mawakala wa forodha ni kiungo muhimu kati ya wafanyabiashara, Serikali, bandari, makampuni ya usafirishaji wa baharini na wadau wengine wa mnyororo wa ugavi. Amesisitiza umuhimu wa uadilifu, usahihi wa taarifa, usiri wa taarifa za wateja na uwajibikaji katika utoaji wa huduma