TASAC YAHITIMISHA MAFUNZO YA KUKABILIANA NA MAJANGA YA MOTO MAHALA PA KAZI
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) tarehe 30 Septemba, 2026 limehitimisha mafunzo ya kukabiliana na majanga ya moto mahala pa kazi, yaliyolenga kuwajengea watumishi uwezo wa kinadharia na vitendo katika kuzuia, kudhibiti na kukabiliana na majanga ya moto yanayoweza kutokea katika maeneo ya kazi.
Akifunga mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa City Garden, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Shirika wa TASAC, Bw. Hamid Mbegu, ameishukuru Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania kwa ushirikiano uliowezesha kufanyika kwa mafunzo hayo, pamoja na wakufunzi kwa kutoa elimu na mafunzo kwa watumishi wa TASAC.
Bw. Mbegu amesema mafunzo hayo yamewajengea watumishi uelewa na ujuzi kuhusu namna ya kuzuia majanga ya moto, matumizi sahihi ya vifaa vya kuzimia moto, pamoja na hatua stahiki za kuchukua wakati wa dharura.
Amesema ujuzi huo ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa watumishi wa kuchukua hatua za haraka na sahihi wakati wa majanga, ikiwa ni pamoja na kulinda maisha ya watu, mali na mazingira ya kazi.
Aidha, amewasisitiza watumishi kutumia elimu na ujuzi walioupata kwa vitendo, kuzingatia taratibu za usalama mahala pa kazi na kuwa tayari kuchukua hatua stahiki pindi hali ya dharura inapojitokeza.
Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za TASAC katika kuimarisha usalama wa watumishi na kuhakikisha mazingira ya kazi yanaendelea kuwa salama na yenye kuzingatia viwango na taratibu za usalama.
Mafunzo hayo yaliyotolewa kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania yamehusisha vipengele vya kinadharia na vitendo, vikiwemo utambuzi na uzuiaji wa vihatarishi vya moto, matumizi sahihi ya vifaa vya kuzimia moto na namna ya kuchukua hatua wakati wa dharura.
Mafunzo hayo pia yanaendana na matakwa ya kisheria na kiusalama yanayohusu usalama na afya mahala pa kazi, ikiwa ni sehemu ya hatua za taasisi kuhakikisha watumishi wanakuwa na uelewa na uwezo wa kukabiliana na majanga ya moto.