Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YASHIRIKI TUKIO LA KIDUNIA LA USAFI WA FUKWE MAGHA, KINONDONI

Imewekwa: 22 September, 2026
TASAC YASHIRIKI TUKIO LA KIDUNIA LA USAFI WA FUKWE MAGHA, KINONDONI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, tarehe 19 Septemba, 2026, limeshiriki zoezi la usafi katika Fukwe za Magha, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha usafi na utunzaji wa mazingira ya bahari na fukwe.

Zoezi hilo lililoandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Human Dignity and Environmental Care Foundation, hufanyika kila mwaka mwezi Septemba, likilenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira ya bahari na fukwe, pamoja na kuendeleza matumizi ya taka kama rasilimali kupitia ubunifu na biashara za kijani.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Msimamizi Mazingira ya Bahari Mwandamizi TASAC, Bw. Julius Salema, amesema ulinzi wa mazingira ya bahari ni wajibu wa kila mwananchi, kwa kuwa afya ya bahari ina uhusiano na afya ya binadamu, uchumi wa buluu na ustawi wa jamii.

Amesema utupaji holela wa nyavu zilizochakaa na taka za plastiki unahatarisha viumbe wa baharini na afya za wananchi.

“Baadhi ya wavuvi wamekuwa wakichoma au kuzika nyavu zilizochakaa kandokando ya bahari. Mawimbi na upepo hurudisha mabaki ya plastiki baharini. Viumbe wa baharini wanapomeza chembe hizo huathirika, na hatimaye binadamu tunapokula samaki hao tunaweza kupata madhara ya kiafya,” amesema.

Aidha, Bw. Salema amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu na kuwawezesha Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMUs) katika majukumu yao ya usimamizi na utunzaji wa rasilimali za bahari.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Human Dignity and Environmental Care Foundation, Bi. Sarah Pima, amesema taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na wadau kuendesha kampeni za usafi wa fukwe, kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira na kugawa vifaa vya usafi kwa jamii za pwani.

“Mwaka huu tumefanikiwa kufanya shughuli hizi katika Fukwe za Kawe kwa ushirikiano mkubwa wa TASAC na wadau wengine,” amesema.

Kauli mbiu ya tukio hilo ni “Blue to Circular Economy: Empowering BMUs Through Beach & Eco Product Innovation.”

Mrejesho, Malalamiko au Wazo