TASAC YASHIRIKI MAONESHO YA 21 YA BIASHARA YA AFRIKA MASHARIKI
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) linashiriki katika Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki (Mwanza East Africa Trade Fair – MEATF), yanayofanyika katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza kuanzia tarehe 28 Agosti hadi 6 Septemba 2026.
Ushiriki wa TASAC unalenga kutoa fursa kwa wananchi, wafanyabiashara na wadau mbalimbali kupata uelewa kuhusu huduma na shughuli zinazotekelezwa na TASAC katika sekta ya usafiri wa majini.
Katika maonesho hayo, TASAC inaendelea kutoa elimu kuhusu majukumu yake kikamilifu, ikiwemo udhibiti wa huduma za usafiri wa majini, usalama wa vyombo vya majini, udhibiti wa shughuli za uwakala wa meli pamoja na masuala ya mazingira katika maeneo ya majini. Pia, wananchi wanapata fursa ya kuwasilisha maoni, maswali na changamoto zinazohusiana na huduma zinazosimamiwa na TASAC.
TASAC inawahimiza wananchi na wadau wa sekta ya usafiri na biashara kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea banda la TASAC, kupata elimu sahihi kuhusu huduma zinazotolewa na majukumu ya taasisi, pamoja na kufahamu namna bora ya kushiriki katika shughuli za usafiri wa majini kwa kuzingatia usalama, ufanisi na utunzaji wa mazingira.
Kaulimbiu ya Maonesha haya ni "Usalama na Amani ni kichocheo cha Biashara na Uwekezaji Hapa nchini."