The United Republic of Tanzania

Tanzania Shipping Agencies Corporation

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YASHIRIKI KIKAO KAZI CHA WATAALAMU WA LOJISTIKI NA USAFIRISHAJI MOROGORO

Posted On: 11 November, 2026
TASAC YASHIRIKI KIKAO KAZI CHA WATAALAMU WA LOJISTIKI NA USAFIRISHAJI MOROGORO

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) linashiriki katika Kikao Kazi cha Wataalamu wa Lojistiki na Usafirishaji Tanzania, kilichoandaliwa na Chama cha Wataalamu wa Lojistiki na Usafirishaji Tanzania (TALTA), kuanzia tarehe 9 hadi 13 Novemba, 2026, katika Hoteli ya Nashera, mkoani Morogoro.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Rais wa TALTA, Bw. Alphonse Mwingira, amewahimiza wataalamu wa lojistiki na usafirishaji kuimarisha ushirikiano katika kuboresha huduma, kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za usafirishaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Amesema kikao hicho kinalenga kujadili maendeleo na changamoto za sekta hiyo, pamoja na umuhimu wa mipango jumuishi na utaalamu katika kuimarisha mifumo ya usafirishaji nchini.

Aidha, amewataka wadau kutambua umuhimu wa sekta ya usafiri wa majini katika kukuza biashara na uchumi, hususan kutokana na ongezeko la shehena katika bandari za Tanzania, linalohitaji ushirikiano wa karibu ili kuongeza ufanisi wa huduma.

Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa TASAC Sirari, Bw. Doctor Kubini, akiwasilisha mada yenye kichwa “Jukumu la Mdhibiti katika Usimamizi wa Usalama na Uendelezaji wa Sekta ya Usafiri wa Majini,” ameeleza nafasi ya udhibiti katika kuhakikisha usalama, uzingatiaji wa sheria na kanuni pamoja na maendeleo endelevu ya sekta hiyo.

Katika majadiliano, wadau wameipongeza TASAC kwa kusimamia usalama wa usafiri wa majini katika Maziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa, hatua inayochangia kulinda maisha ya abiria, usalama wa mizigo na shughuli za kiuchumi.

Vilevile, wamepongeza juhudi za TASAC katika kusimamia na kudhibiti shughuli za biashara, ikiwemo ukaguzi wa kampuni za mawakala wa forodha na mawakala wa meli, ili kuhakikisha uzingatiaji wa sheria na taratibu, ushindani wa haki na kulinda maslahi ya Watanzania.

Kikao hicho kinatarajiwa kuhitimishwa tarehe 13 Novemba, 2026, na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Prof. Shemdoe.

Feedback, Complaint or Opinion