Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

KAMATI YA PIC YAPONGEZA UTENDAJI KAZI WA TASAC, YAUNGA MKONO UANZISHWAJI WA TaMA

Imewekwa: 09 November, 2026
KAMATI YA PIC YAPONGEZA UTENDAJI KAZI WA TASAC, YAUNGA MKONO UANZISHWAJI WA TaMA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), leo tarehe 8 Novemba, 2026, jijini Dar es Salaam  imekutana na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), kujadili utekelezaji wa majukumu, mafanikio na mipango ya kimkakati ya TASAC.

Akizungumza katika ziara hiyo Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Elibariki Kingu, ameipongeza TASAC kwa kusimamia na kudhibiti sekta ya usafiri majini, akieleza kuwa mafanikio yaliyofikiwa yanaonesha mchango wa Shirika katika maendeleo ya sekta ya uchukuzi na uchumi wa taifa. 

Mhe. Kingu amesema Kamati itaunga mkono juhudi za Serikali za kuanzisha Mamlaka ya Usafiri Majini Tanzania (TaMA), akieleza umuhimu wa mageuzi hayo katika kuimarisha usimamizi na udhibiti wa sekta ya usafiri majini nchini.

Akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi ya Shirika, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, amesema makusanyo ya mapato yameongezeka kutoka shilingi bilioni 47.39 mwaka 2018/19 kufikia bilioni 110.40 mwaka 2025/26, huku TASAC ikichangia jumla ya shilingi bilioni 169.39 katika Mfuko Mkuu wa Serikali kuanzia mwaka 2019/20 hadi 2025/26.

Ametaja miradi ya kimkakati iliyotekelezwa na TASAC ni pamoja na Kituo cha Kikanda cha Uratibu wa Utafutaji na Uokoaji na vituo vidogo vya uokoaji, boti za uokoaji na matibabu pamoja na mifumo ya TEHAMA.

Bw. Salum ameongeza kuwa Mpango Mkakati wa 2026/27–2030/31 unalenga kuimarisha usalama, mageuzi ya kidijitali, uendelevu wa kifedha na Uchumi wa Buluu. 

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC, Nahodha Mussa Mandia, amewashukuru wajumbe wa Kamati kwa ziara hiyo, na ameishukuru Kamati kwa utayari wa kusaidia uanzishwaji wa TaMA.

Akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Hazina, Bi. Lightness Mauki, amesema TASAC ni miongoni mwa taasisi zinazofanya vizuri, hali iliyochangia kutunukiwa Tuzo ya Taasisi Bora kwa Uzingatiaji wa Sheria (Most Compliant Institution).

Ziara hiyo ni sehemu ya jukumu la Kamati la kufuatilia utendaji wa taasisi za umma, matumizi ya rasilimali na mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo