TASAC YAPONGEZWA UDHIBITI WA UCHAFUZI WA MAZINGIRA YA BAHARI
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Reuben Kwagilwa ameipongeza TASAC kwa mchango wake mkubwa katika kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwenye sekta ya usafiri majini pamoja na na kulinda mazingira ya bahari, maziwa na mito nchini.
Ametoa pongezi hizo tarehe 1 Juni 2026 jijini Dodoma wakati alipotembelea Banda la TASAC wakati wa hafla ya uzinduzi wa Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC).
Aidha, aliitaka TASAC kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kuibua miradi ya utunzaji wa mazingira ya baharini kupitia fursa za miradi ya 'Net Zero Emission', GCF, 'Carbon Credits' na 'Marine Decarbonization'.
Mhe. Kwagilwa alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, taasisi mbalimbali na jamii katika kukabiliana na changamoto za mazingira, hususan mabadiliko ya tabianchi. Alieleza kuwa ushirikiano wa wadau ni msingi wa kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.
Maonesho ya Siku ya Mazingira yamelenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Dira 2050, Tuwajibike Kukijanisha Tanzania”, ikisisitiza wajibu wa kila Mtanzania kushiriki katika uhifadhi wa mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.