TASAC YAPONGEZWA NA TPA KWA UBORA WA HUDUMA NA USHIRIKIANO
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limepongezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa ubora wa huduma kwa wateja, ushirikiano na uaminifu katika kutekeleza majukumu yake ndani ya sekta ya usafiri majini nchini.
Pongezi hizo zimetolewa, leo tarehe 27 Oktoba, 2026 na Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed Gallus, wakati akikabidhi Tuzo ya Ubora katika Huduma kwa Wateja (Customer Service Excellence Award) na Cheti cha Pongezi zilizotolewa kwa TASAC kwa kutambua ushirikiano mzuri na uhusiano endelevu kati ya taasisi hizo.
Bw. Gallus ameongeza kuwa TPA imetambua mchango wa TASAC katika kuimarisha na kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika sekta ya usafiri kwa njia ya maji nchini hali iliyochangia ongezeko la shehena inayopita katika Bandari ya Dar es Salaam.
Akipokea tuzo hizo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, CPA Pascal Karomba, ameishukuru Bandari ya Dar es Salaam kwa kutambua mchango wa TASAC na kuthamini ushirikiano uliopo kati ya taasisi hizo.
CPA Karomba ameeleza kuwa Bandari ya Dar es Salaam ni mdau mkuu wa TASAC, hususan katika kufanikisha usafirishaji kwa njia ya maji nchini. Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano huo ili kuongeza ufanisi wa huduma na kuchochea maendeleo ya sekta ya usafiri majini.
Ameongeza kuwa tuzo na cheti hicho ni chachu kwa TASAC kuendelea kudumisha uaminifu, kuimarisha ushirikiano na kuboresha huduma kwa manufaa ya wadau na Taifa kwa ujumla.
TASAC inaendelea kushirikiana na TPA pamoja na wadau wengine kuhakikisha kuwa huduma za usafiri majini zinaimarika, zinazingatia viwango vinavyotakiwa na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.