TASAC YAKUTANA NA WADAU KUJADILI MABORESHO YA HUDUMA ZA BANDARI
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limefanya kikao cha mashauriano na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji na biashara kwa lengo la kujadili masuala yaliyoibuliwa wakati wa ziara yake nchini Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kikao hicho kilifanyika leo, Juni 3, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa LATRA. Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafirishaji Majini, Bw. Silvester Kanyika alisema kuwa juhudi zote zinazofanywa na TASAC zinalenga kuboresha ufanisi wa shughuli za bandari na kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa kuzingatia misingi thabiti ya utendaji, ikiwemo matumizi ya lugha nzuri kwa wateja.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Zahor Salum kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) alisema kuwa taasisi hiyo iko tayari kushirikiana na TASAC katika utekelezaji wa mfumo wa Single Customs Territory ili kurahisisha taratibu za usafirishaji wa mizigo na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma.
“TRA ina wataalamu wa kutosha ambao wako tayari kutoa elimu kwa wadau mbalimbali. Ushirikiano huu utasaidia kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma,” alisema Bw. Salum.
Kwa upande wake, Bw. Lukindo Josephat kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) alisema kuwa TPA inaendelea kufanya jitihada za kupunguza baadhi ya tozo za bandari ili kuongeza ushindani wa bandari za Tanzania na kuwavutia zaidi wafanyabiashara kutumia huduma zake.
Naye Bw. Lihami Masoli kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) alisema kuwa TRC imejipanga kutoa treni na mabehewa kwa ajili ya kusafirisha mizigo kati ya Uganda na Tanzania. Aidha, shirika hilo linaendelea kuweka mifumo ya ufuatiliaji wa mizigo (trackers) kwenye mabehewa ili kurahisisha ufuatiliaji wa mizigo katika safari zake.
Akihitimisha kikao hicho, Bw. Kanyika alisema TASAC itaendelea kushirikiana kwa karibu na TPA, TRA na TRC katika kutekeleza maazimio yaliyofikiwa, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo, ili kuimarisha ushindani wa bandari za Tanzania katika soko la kimataifa na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.