TASAC YAIBUKA MSHINDI WA TATU KATIKA MAONESHO YA 21 YA BIASHARA AFRIKA MASHARIKI (MEATF)
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeibuka mshindi wa tatu katika kundi la Taasisi za Wakala za Serikali wakati wa ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki (MEATF), yanayofanyika katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.
Ushindi huo unaifanya TASAC kutambuliwa miongoni mwa taasisi zilizofanya vizuri katika maonesho hayo, ambayo yanalenga kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki na Bara la Afrika kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho hayo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, amesema Serikali inalenga kuifanya Tanzania ipige hatua kutoka kuwa soko la bidhaa kutoka nje na kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
“Tunataka Tanzania isiwe soko pekee la bidhaa; tunataka iwe kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa katika Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla,” amesema Mhe. Londo.
Ameongeza kuwa maonesho ya biashara kama MEATF yana nafasi muhimu katika kuwaunganisha wazalishaji, wafanyabiashara, wawekezaji na wadau mbalimbali wa sekta ya biashara, sambamba na kutoa fursa ya kutangaza bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.
TASAC kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo imeendelea kutoa elimu na taarifa kwa wananchi na wadau kuhusu majukumu na huduma zake katika sekta ya usafiri wa majini. Aidha, Shirika limeendelea kujenga uelewa kuhusu mchango wake katika usimamizi wa shughuli za usafiri majini, usalama na ulinzi, utunzaji wa mazingira ya bahari na maziwa pamoja na kuwezesha mazingira salama na yenye ufanisi kwa shughuli za biashara zinazotegemea usafiri wa majini.
Maonesho hayo yanafanyika chini ya kaulimbiu “Usalama na Amani ni Kichocheo cha Biashara na Uwekezaji Hapa Nchini. Yalianza tarehe 28 Agosti 2026 na yanatarajiwa kufikia tamati tarehe 6 Septemba 2026.