Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAENDELEA KUTOA MAFUNZO KUHUSU MFUMO MPYA WA MTRS

Imewekwa: 06 September, 2026
TASAC YAENDELEA KUTOA MAFUNZO KUHUSU MFUMO MPYA WA MTRS

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeendelea kutoa mafunzo kwa wadau wa sekta ya usafiri majini kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa kielektroniki wa Maritime Transport Regulatory System (MTRS), unaolenga kuboresha utoaji wa huduma za udhibiti katika sekta hiyo.

Mafunzo hayo yalitolewa Septemba 1, 2026 katika Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Sirari One Stop Border Post, na kufunguliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhe. Meja Edward Gowele.

Mfumo wa MTRS ulianza kutumika rasmi Septemba 1, 2026, ukichukua nafasi ya mfumo uliokuwa ukitumika awali wa Manifest Billing System (MBILL).

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Gowele amesema matumizi ya mfumo mpya wa MTRS yanatarajiwa kuongeza ufanisi, uwazi na urahisi katika utoaji wa huduma mbalimbali za udhibiti, ikiwemo utoaji wa leseni na usajili kwa watoa huduma katika sekta ya usafiri majini.

Amesema matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wadau bila kulazimika kutumia muda mwingi kufuatilia taratibu kwa njia za kawaida.

Kupitia mfumo huo, TASAC imeeleza kuwa watoa huduma wataweza kuomba leseni na vyeti vya usajili, kuwasilisha nyaraka zinazohitajika, kufuatilia hatua za maombi yao pamoja na kupata taarifa mbalimbali kwa njia ya mtandao.

Aidha, matumizi ya MTRS yanatarajiwa kupunguza utegemezi wa nyaraka za karatasi, kurahisisha mawasiliano kati ya TASAC na wadau pamoja na kupunguza muda unaotumika katika kufuatilia na kupata huduma.

TASAC inaendelea kutoa mafunzo kwa wadau katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha watumiaji wa mfumo wanauelewa na kuutumia kwa ufanisi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Shirika za kuimarisha huduma za kidijitali na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma katika sekta ya usafiri majini.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo