Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAFANYA MKUTANO MKUU WA MWAKA WA WAFANYAKAZI

Imewekwa: 02 November, 2026
TASAC YAFANYA MKUTANO MKUU WA MWAKA WA WAFANYAKAZI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 30 Oktoba, 2026 limefanya Mkutano wa Mwaka wa Wafanyakazi kwa lengo la kujadili mwelekeo wa kimkakati wa Shirika, mafanikio yaliyopatikana na mipango ya utekelezaji wa majukumu yake.

Akizungumza katika Mkutano huo uliofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha, Pwani, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/26 Shirika limefanikiwa kukusanya mapato yanayofikia shilingi bilioni 110.4 kutoka shilingi bilioni 90.1 za mwaka wa fedha 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 22.5.

Bw. Salum ameongeza kuwa TASAC ipo katika mchakato wa kubadilisha hadhi yake kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania kwenda kuwa Mamlaka ya Usafiri wa Majini Tanzania (TaMA), hatua inayolenga kuimarisha mfumo wa udhibiti wa sekta ya usafiri majini nchini. 

Mkutano huo pia umejadili maboresho ya mazingira ya kazi, maandalizi ya ujenzi wa jengo la Makao Makuu, matumizi ya mifumo ya TEHAMA pamoja na juhudi za kuimarisha huduma za usalama, ulinzi na utafutaji na uokoaji majini.

Aidha, Bw. Salum amesisitiza umuhimu wa kila mtumishi kutambua wajibu wake, kuweka mbele maslahi ya Shirika na kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bibi Susan Mlawi amewaelekeza watumishi wa TASAC kutoa huduma bora kwa wateja kwa kuzingatia misingi ya heshima, uwazi, ufanisi na uwajibikaji. 

Ameeleza umuhimu wa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na kuwakumbusha kuwa wanapaswa kuzingatia maadili na taratibu za utumishi wa umma wanapotumia majukwaa hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa COTWU (T), Tawi la TASAC, Bw. Mohamed Kapera, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Menejimenti na wafanyakazi. Ameiomba Menejimenti ya TASAC kuzingatia kuboresha maslahi, motisha, mazingira ya kazi na ustawi wa wafanyakazi, huku akihimiza majadiliano ya kujenga kwa maendeleo ya Shirika.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo