TASAC YAENDELEZA UTAMADUNI WA MAZOEZI KUPITIA BONANZA LA MICHEZO
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 31 Oktoba 2026, limefanya Bonanza la Michezo katika Viwanja vya Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha, mkoani Pwani, kwa lengo la kuimarisha afya za watumishi, kuongeza mshikamano, umoja na mahusiano mema kazini.
Bonanza hilo limewashirikisha watumishi wa TASAC pamoja na timu kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani na Viongozi wa Klabu ya Michezo ya Wizara ya Uchukuzi likitoa fursa ya kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizo kupitia michezo.
Akifungua bonanza hilo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mkurugenzi wa Udhibiti na Usimamizi wa Huduma za Usafiri Majini, Bw. Nelson Mlali, amewapongeza washiriki kwa kujitokeza na kuwataka kufanya michezo na mazoezi kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku ili kujenga afya bora na kuongeza ufanisi kazini.
Amesisitiza kuwa bonanza hilo ni mwendelezo wa utekekezaji wa mada zilizotolewa wakati wa mkutano wa Wafanyakazi kuhusu uzingatiaji wa taratibu za kiafya na kujenga nidhamu mahala pa kazi. Alisisitiza kuwa; michezo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha ushirikiano, kupunguza msongo wa mawazo na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa watumishi, huku akiwahimiza kudumisha upendo na moyo wa kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao.
Aliwataka washiriki wote kukuza utamaduni wa michezo katika familia zao pia. Alimalizia kwa kumtaka kila mwana TASAC kuachia kiti na kutenga muda wa kushiriki mazoezi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Shirika, Bw. Hamid Mbegu, amezipongeza taasisi zilizoshiriki pamoja na uongozi mzima wa Chuo cha Mwalimu Nyerere kwa ushirikiano waliouonesha.
Aidha ameishukuru Kamati ya Maandalizi na kuwataka watumishi kuimarisha ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja ili kuongeza ufanisi wa Shirika. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maelekezo ya Serikali kuhusu ushiriki katika michezo na mazoezi ya mwili kwa ajili ya kuboresha afya, ustawi na kuongeza tija katika utumishi wa umma.
Bonanza hilo limehusisha michezo mbalimbali ikiwemo riadha, mpira wa miguu, kuvuta kamba, kukimbiza kuku pamoja na michezo ya jadi ya bao na karata, iliyowapa washiriki fursa ya kujumuika na kuburudika.
Kupitia bonanza hilo, TASAC inaendelea kuhamasisha utamaduni wa mazoezi na michezo, ikitambua kuwa afya bora, mshikamano na mahusiano mazuri kazini ni msingi wa kuongeza ari, morali na ufanisi katika utendaji wa kazi.