Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC, NBS WAFANYA MAJARIBIO YA SENSA PWANI YA BAGAMOYO

Imewekwa: 30 September, 2026
TASAC, NBS WAFANYA MAJARIBIO YA SENSA PWANI YA BAGAMOYO

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), leo tarehe 29 Septemba, 2026 wamefanya zoezi la majaribio ya Sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini na Wajenzi wa Meli Tanzania Bara kwa mwaka 2026, katika maeneo ya Pwani ya Bagamoyo.

Zoezi hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha zoezi la Sensa linafanyika kwa ufanisi, kwa maafisa Sensa  kutekeleza kwa vitendo mafunzo waliyopatiwa.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Nahodha Alex Katama, Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam Wanaoratibu Zoezi la Sensa, amesema kuwa zoezi la majaribio limeenda vizuri na washiriki wameweza kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maelekezo na mafunzo waliyopatiwa.

Amesema Maafisa Sensa wamepata fursa ya kufanya majaribio ya vitendo, hatua ambayo imewasaidia kujenga uelewa na uzoefu wa namna ya kukusanya taarifa sahihi za Sensa kutoka kwa wamiliki na waendeshaji wa vyombo na maeneo ya ujenzi wa vyombo.

“Kwa ujumla, zoezi limeenda vizuri. Maafisa Sensa  wameweza kufanya majaribio kama walivyofundishwa, jambo ambalo linaonesha kuwa  wako  tayari kutekeleza zoezi la Sensa kwa ufanisi,” amesema Nahodha Katama.

Kwa upande wao, wavuvi pamoja na wajenzi wa vyombo vya usafiri majini walieleza utayari wao wa kutoa ushirikiano katika zoezi hilo, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa zinazohitajika ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi na zenye ubora kuhusu sekta ya usafiri majini nchini.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuwa chachu katika kufanikisha Sensa hiyo, ambayo inalenga kupata taarifa muhimu kuhusu idadi na aina ya vyombo vya usafiri majini pamoja na shughuli za ujenzi wa meli na vyombo vingine vya majini Tanzania Bara.

TASAC na NBS zimeendelea kuhamasisha wadau wote kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati, ili kuwezesha Serikali kupata takwimu zitakazosaidia katika kupanga, kusimamia na kuendeleza sekta ya usafiri majini nchini.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo