TASAC NA NBS KUSHIRIKIANA KUTEKELEZA SENSA YA VYOMBO VYA USAFIRI MAJINI NA WAJENZI WA MELI TANZANIA BARA 2026/27
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) leo, tarehe 3 Juni, 2026, zimesaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) yatakayowezesha maandalizi na utekelezaji wa Sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini, Maeneo ya Ujenzi wa Meli na Wajenzi wa Meli Tanzania Bara kwa mwaka 2026/27.
Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha upatikanaji wa takwimu sahihi, za kuaminika na za kisasa zitakazosaidia kupanga, kusimamia na kuendeleza sekta ya usafiri majini nchini. Sensa hiyo itakuwa ya pili kufanyika nchini baada ya sensa ya kwanza iliyotekelezwa mwaka 2021 kwa ushirikiano wa TASAC na NBS.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, amesema sensa hiyo ni hatua muhimu katika kuhuisha kanzidata ya kitaifa ya vyombo vya usafiri majini na kupata taarifa sahihi kuhusu vyombo vinavyofanya kazi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara.
Bw. Salum ameongeza kuwa matokeo ya sensa yatasaidia kuboresha usimamizi wa usalama majini, kuimarisha utekelezaji wa sheria na kanuni, pamoja na kusaidia maamuzi ya kisera, kiudhibiti na kiuwekezaji katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, amesema sensa hiyo itasaidia utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya Serikali, ikiwemo kuimarisha mfumo wa usafirishaji fungamanishi nchini. Amesema takwimu zinazopatikana kupitia sensa ni nyenzo muhimu katika kufanya maamuzi sahihi ya kisera, kupanga uwekezaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha, ameilishukuru TASAC kwa kuendelea kushirikiana na NBS katika utekelezaji wa zoezi hilo muhimu, akieleza kuwa ushirikiano huo unaimarisha juhudi za Serikali za kuhakikisha upatikanaji wa takwimu bora, za kuaminika na zinazokidhi mahitaji ya maendeleo ya Taifa.
Takwimu zitakazopatikana zitatumika kuimarisha usalama wa vyombo na abiria, kuboresha upangaji wa miundombinu ya usafiri majini, kuchochea uwekezaji katika uchumi wa buluu na kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.