Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC KINARA WA TUZO ZA NBAA, YAAHIDI KUENDELEZA UFANISI WA USIMAMIZI WA FEDHA

Imewekwa: 27 November, 2026
TASAC KINARA WA TUZO ZA NBAA, YAAHIDI KUENDELEZA UFANISI WA USIMAMIZI WA FEDHA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeendelea kuthibitisha ubora wake katika usimamizi wa fedha baada ya kushika nafasi ya kwanza katika Tuzo za Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), katika uandaaji wa taarifa za fedha zinazokidhi viwango vya kimataifa.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Fedha wa TASAC, CPA Pascal Karomba, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, leo Novemba 26, 2026, katika ukumbi wa Hoteli ya APC, jijini Dar es Salaam, amesema tuzo hiyo ni heshima kwa Shirika na inaakisi uimara wa mifumo ya kifedha, uwazi na uzingatiaji wa viwango vya kitaaluma pamoja na sheria na taratibu za matumizi ya fedha za umma.

Ameongeza kuwa mafanikio hayo yameendelea kuimarisha imani ya wadau wa sekta ya usafiri wa majini na wananchi kwa ujumla, kutokana na uandaaji wa taarifa za fedha unaozingatia taratibu, sheria na kanuni zinazotakiwa.

“Tuzo hii inatupa motisha ya kuendelea kuboresha utendaji, kuimarisha mifumo ya udhibiti wa vihatarishi na kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kwa tija na ufanisi katika kuhudumia wananchi,” amesema CPA Karomba.

Aidha, amesema TASAC imeendelea kushika nafasi ya kwanza kwa mara ya sita, mafanikio yanayoipa motisha ya kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma na kuzingatia misingi ya mazingira, jamii na utawala bora ili kudumisha uwajibikaji.

Wakati huo huo, mgeni rasmi katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha (Huduma za Hazina), Nsubili Joshua, amewapongeza washindi kwa kuandaa taarifa za fedha zenye ubora na zinazozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.

Amesema taarifa hizo zinaonesha uwajibikaji wa viongozi katika kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi, uwazi na manufaa ya wananchi, akisisitiza kuwa uandaaji sahihi wa taarifa za fedha ni nyenzo muhimu katika kuimarisha utawala bora na kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi za umma.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo