MAADHIMISHO YA PILI YA WIKI YA USAFIRI ENDELEVU ARDHINI 2026 YAFUNGWA RASMI
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Usafiri wa Barabara, Wizara ya Uchukuzi, Bw. Andrew Magombana, amefunga rasmi Maadhimisho ya Pili ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2026, akisisitiza umuhimu wa jukwaa hilo katika kuwakutanisha wadau wa sekta ya uchukuzi na wananchi kujadili fursa, changamoto na mikakati ya pamoja ya kuboresha huduma za usafiri nchini.
Akizungumza katika hafla ya kufunga maadhimisho hayo iliyofanyika Novemba 26, 2026, katika viwanja vya Mlimani City, jijini Dar es Salaam, Magombana amesema maadhimisho hayo ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na kujadili mikakati inayolenga kuboresha huduma za usafiri, kuimarisha usalama na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Maadhimisho haya ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa sekta ya usafiri ardhini, kubadilishana uzoefu na kujadili mikakati ya pamoja itakayosaidia kuboresha huduma za usafiri, kuimarisha usalama na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” amesema Magombana.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia usafiri jumuishi kwa kuendeleza mifumo ya usafiri inayokidhi mahitaji ya wananchi wote, sambamba na kuimarisha sekta ya uchukuzi kama kichocheo cha biashara, uwekezaji na maendeleo ya Taifa.
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeshiriki katika hafla hiyo ya kufunga maadhimisho yaliyofanyika kuanzia Novemba 16 hadi 26, 2026, yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi.
Kupitia ushiriki wake, TASAC imeendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano baina ya sekta ya usafiri wa majini na usafiri wa ardhini katika kuimarisha mnyororo wa usafirishaji, kukuza biashara na kuongeza ufanisi wa huduma za uchukuzi.
Maadhimisho hayo yalilenga kuhamasisha matumizi ya mifumo endelevu ya usafiri na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wadau wa sekta ya uchukuzi nchini. Kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa “Kuharakisha Usafiri Endelevu: Usafiri Salama, Rafiki kwa Mazingira na Jumuishi kwa Wote” (Accelerating Sustainable Transport: Safe, Green and Inclusive Mobility).