TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA TATU WA UN KUHUSU NCHI ZISIZO NA BANDARI

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashiriki Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Nchi Zisizo na Mlango wa Bahari (Bandari) ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano huo unaofanyika Awaza, nchini Turkmenistan tarehe 5 – 8 Agosti, 2025.
Akifungua Mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Turkmenstan, Mhe. Serdar Berdimuhamedow amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, hasa ushirikiano wa nchi za Kusini kwa Kusini katika kukabiliana na changamoto za kipekee zinazozikumba nchi zisizo na bandari na kutoa wito wa ushirikishwaji jumuishi unaohusisha Serikali, mabunge, vijana, na asasi za kiraia.
Alitumia mkutano huo kuthibitisha msimamo wa Turkmenistan wa kutokuegemea upande wowote na kueleleza kuunga mkono utekelezaji wa Mpango wa maendeleo wa mwaka 2024–2034 wenye lengo la kukuza miunganisho, ustahimilivu na maendeleo endelevu kwa nchi zisizo na bandari.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano huo, Katibu Mkuu wa UN, Mhe. António Guterres, alisisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa wenye nguvu na wa vitendo ni muhimu zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote kwa kuwa changamoto za dunia kama za mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kiuchumi, na miundombinu hafifu zinahitaji majibu ya pamoja, hasa kwa nchi zisizo na bandari.
Alihimiza ushirikiano jumuishi katika uwekezaji wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2024–2034.
Mkutano huo unatarajiwa kutoa Tamko la Kisiasa la Awaza na mpango kazi mpya wa kimataifa wa miaka 10 kwa Nchi zisizo na Bandari utakaolenga kuboresha muunganiko wa miundombinu kati ya nchi zisizo na bandari na zile zenye bandari, kuweka mazingira wezeshi kwa biashara, uwekezaji, na huduma za usafirishaji, pamoja na kuhimiza matumizi ya teknolojia na dijitali katika kuboresha huduma za mipaka na ufanisi wa biashara na kuimarisha usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa vijana na ushirikiano wa sekta binafsi.
Kauli mbiu ya Mkutano huo ni: “Kufungua Fursa kwa Nchi Zisizo na Bahari kwa Maendeleo Endelevu kupitia Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa”.