Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TANZANIA YASAINI MKATABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU NYARAKA ZA USAFIRISHAJI WA MIZIGO

Imewekwa: 28 October, 2026
TANZANIA YASAINI MKATABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU NYARAKA ZA USAFIRISHAJI WA MIZIGO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo tarehe 26 Oktoba 2026 imesaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Nyaraka za Usafirishaji wa Mizigo (United Nations Convention on Negotiable Cargo Documents), unaojulikana kama Accra Convention, katika hafla iliyofanyika jijini Accra, Ghana.

Mkataba huo umesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, kufuatia mamlaka aliyopewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.).

Mkataba huo unalenga kuwezesha usafiri fungamanishi wa mizigo (multimodal transport) unaounganisha njia za majini, barabara, reli na anga kupitia matumizi ya nyaraka za usafirishaji zinazotambulika kisheria. Mkataba huo unawezesha uhamishaji wa haki za umiliki wa mizigo na kusaidia wafanyabiashara kupata ufadhili kutoka taasisi za kifedha, kwa kuzingatia masharti husika.

Aidha, utekelezaji wa Mkataba unatarajiwa kusaidia kupunguza urudufu wa nyaraka, muda na gharama za usafirishaji, kurahisisha taratibu za biashara na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali.

Hatua hii inaendana na malengo ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA), Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango Mkakati wa TASAC katika kuboresha huduma za usafirishaji na kuongeza ushindani wa Tanzania katika biashara ya kikanda na kimataifa, hususan kwa kuimarisha ufanisi na ushindani wa bandari za Tanzania.

Baada ya utiaji saini, Tanzania itafuata taratibu za kitaifa za kuridhia Mkataba huo kwa mujibu wa sheria zinazotumika. Kuanza kutumika kwa Mkataba huo kutaimarisha sekta ya usafirishaji na kuendeleza Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafiri katika Afrika Mashariki na Kati.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo