Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TAHADHARI YA EL NIÑO: MTWARA WAASWA KUCHUKUA TAHADHARI

Imewekwa: 22 September, 2026
TAHADHARI YA EL NIÑO: MTWARA WAASWA KUCHUKUA TAHADHARI

Wavuvi mkoani Mtwara wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa na dhoruba zinazoweza kuambatana na hali ya hewa ya El Niño, kwa kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa kabla ya kwenda baharini.

Wito huo umetolewa na Afisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Kanda ya Kusini, Mhandisi Joseph Myaka, wakati akitoa elimu ya tahadhari dhidi ya athari za El Niño kwa wavuvi katika eneo la Feri, Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara.

Mhandisi Myaka amesema wavuvi wanapaswa kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kuhakikisha wanakuwa na vifaa muhimu vya usalama, ikiwemo jaketi okozi, pamoja na kufanya shughuli zao katika maeneo yenye mtandao wa simu ili kurahisisha utoaji wa taarifa za dharura endapo watakumbwa na changamoto baharini.

Aidha, amewataka wavuvi kuzingatia masharti ya usalama wa usafiri wa majini na kuepuka kwenda baharini wakati taarifa za hali ya hewa zinaonesha uwepo wa hatari, akisisitiza kuwa usalama wa maisha unapaswa kupewa kipaumbele wakati wote.

Ameongeza kuwa wamiliki na waendeshaji wa vyombo wanatakiwa kuhakikisha vyombo vyao viko katika hali salama, vinafanyiwa ukaguzi unaohitajika na kuwa na vifaa muhimu vya usalama na uokoaji, ikiwemo jaketi okozi (life jackets) za kutosha kwa abiria na wahudumu.

Mhandisi Myaka ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha waendeshaji kutopakia abiria au mizigo kupita uwezo uliowekwa.

Kwa upande wao, baadhi ya wavuvi walioshiriki katika zoezi hilo la utoaji elimu wamesema wataendelea kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na El Niño, huku wakiiomba Serikali kuimarisha huduma za uokoaji baharini kwa kuwapatia boti maalumu za uokoaji ili kusaidia kukabiliana na matukio ya dharura.

Elimu hiyo ni sehemu ya jitihada za TASAC za kuongeza uelewa kwa wadau wa usafiri wa majini kuhusu hatua za kuchukua katika kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na hali ya hewa ya El Niño.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo