Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

RAIS MWINYI AZINDUA MAONESHO YA TAMASHA LA KIZIMKAZI 2026, TASAC YASHIRIKI

Imewekwa: 12 August, 2026
RAIS MWINYI AZINDUA MAONESHO YA TAMASHA LA KIZIMKAZI 2026, TASAC YASHIRIKI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, leo tarehe 12 Agosti 2026, amezindua rasmi Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi 2026 yanayofanyika katika Uwanja wa Dimbani, Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja.

Maonesho hayo, yanayofanyika kuanzia tarehe 12 hadi 14 Agosti 2026, yamebeba kaulimbiu isemayo, “Kizimkazi Kumenoga: Shangwe na Fursa.”

Tamasha hilo limewakutanisha wananchi, viongozi wa Serikali, taasisi za umma na binafsi, wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali kwa lengo la kuonesha shughuli za maendeleo, fursa za kiuchumi, utalii, biashara, utamaduni na huduma mbalimbali zinazotolewa kwa jamii.

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika maonesho hayo, likitoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake ya kusimamia na kudhibiti usafiri kwa njia ya maji ili uwe salama, wenye ufanisi, shindani na rafiki kwa mazingira.

Kupitia Banda lake, TASAC inatoa elimu kuhusu usalama wa vyombo vya majini, abiria, mabaharia na shehena; usajili na ukaguzi wa vyombo; mafunzo na uthibitishaji wa mabaharia; utafutaji na uokoaji; pamoja na ulinzi wa mazingira dhidi ya uchafuzi unaotokana na shughuli za usafiri majini.

Aidha, wananchi na wadau wanaotembelea banda la TASAC wanapata fursa ya kuuliza maswali, kutoa maoni na kupata ufafanuzi kuhusu taratibu za udhibiti wa sekta ya usafiri majini na huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika.

Ushiriki wa TASAC katika Tamasha la Kizimkazi unaimarisha jitihada za Serikali za kukuza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa usafiri salama na endelevu majini katika kuchochea biashara, uvuvi, utalii na maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo