Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

PROF. MBARAWA: MV MWANZA KUANZA KAZI BAADA YA TASAC KUTHIBITISHA USALAMA WAKE

Imewekwa: 27 November, 2026
PROF. MBARAWA: MV MWANZA KUANZA KAZI BAADA YA TASAC KUTHIBITISHA USALAMA WAKE

Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, amesema meli ya MV Mwanza haitarejea kutoa huduma hadi Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) litakapokamilisha ukaguzi na kuthibitisha usalama wake, kufuatia ajali ya meli hiyo kugonga mwamba katika Ziwa Victoria.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, tarehe 26 Novemba, 2026, Waziri Mbarawa amesema uchunguzi wa awali umeonesha kuwa ajali hiyo ilisababishwa na makosa ya kibinadamu (Human Error), huku Serikali ikielekeza hatua za kiufundi, kiutawala na kinidhamu kuchukuliwa ili kuimarisha usalama wa usafiri wa majini.

Mhe. Prof. Mbarawa ameielekeza TASAC kujiridhisha kuwa meli hiyo pamoja na mifumo yake ya uendeshaji na usalama vinakidhi viwango vinavyotakiwa kabla ya kuruhusiwa kurejea kutoa huduma.

Aidha, ameelekeza nahodha aliyekuwa akiendesha meli wakati wa ajali kusimamishwa mara moja na kuchukuliwa hatua stahiki za kiutawala na kinidhamu kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma.

Ameielekeza Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (TASHICO) kufanya matengenezo ya eneo la mbele la meli lililoharibika.

Vilevile, ameitaka TASAC kusimamia kwa karibu utekelezaji wa maagizo hayo na kuhakikisha watumishi wanaohusika na uendeshaji wa meli wanakuwa na taaluma, ujuzi na uwezo unaostahili ili kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viwango vya usalama.

Mhe. Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa usalama wa meli, abiria na wafanyakazi unategemea pia uwajibikaji wa nahodha, akieleza kuwa nahodha anapaswa kufahamu majukumu yake na kufanya maamuzi sahihi wakati wa uendeshaji wa meli.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia usalama wa usafiri wa majini kwa kuhakikisha meli zinazotoa huduma kwa wananchi zinakidhi matakwa na viwango vinavyotakiwa vya usalama.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo