MKURUGENZI TASAC AWAKARIBISHA WANANCHI KIZIMKAZI, ASISITIZA ELIMU YA USALAMA WA USAFIRI MAJINI
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea Banda la TASAC katika Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi 2026, yaliyoanza leo tarehe 12 hadi 14 Agosti, 2026, katika Viwanja vya Maonesho Dimbani, Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja.
Akizungumza katika Maonesho hayo, Bw. Salum amesema ushiriki wa TASAC unalenga kutoa elimu na huduma kwa wananchi na wadau ili waweze kufahamu kwa undani majukumu ya Shirika katika kusimamia na kudhibiti sekta ya usafiri majini nchini.
Amesema wananchi wanaotembelea Banda la TASAC watapata elimu kuhusu usalama na ulinzi wa usafiri majini, usajili wa meli na vyombo vya majini, utoaji wa leseni na vyeti kwa wadau wa sekta hiyo pamoja na masuala ya ulinzi wa mazingira ya bahari.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kupata elimu na ufafanuzi kuhusu huduma za TASAC na namna Shirika linavyotekeleza majukumu yake kwa manufaa ya sekta ya usafiri majini na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu amepata fursa ya kutembelea mabanda ya taasisi mbalimbali zinazoshiriki katika Tamasha la Kizimkazi na kujionea huduma na shughuli zinzotolewa na taasisi hizo.