MKURUGENZI MKUU WA TASAC AHANI KIFO CHA PHILIP GASPAR MSAFIRI
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, leo, tarehe 1 Agosti 2026, amefika nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya kuhani na kutoa salamu za pole kwa familia ya marehemu Phillip Gaspar Msafiri, aliyekuwa Mchumi Mwandamizi katika Kitengo cha Udhibiti Uchumi.
Bw. Salum ameungana na familia, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na watumishi wa Shirika kuomboleza kifo cha Phillip Gaspar Msafiri, na ameeleza kuwa TASAC imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo chake kilichotokea jijini Dar es Salaam.
Bw. Salum amesema marehemu Msafri alikuwa mtumishi mwenye bidii, nidhamu, weledi na moyo wa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake. Ameeleza kuwa kifo chake kimeacha pengo kubwa kwa familia, watumishi wenzake na Shirika kwa ujumla.
Mkurugenzi Mkuu amemuomba Mwenyezi Mungu kuipa familia ya marehemu nguvu, subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Aidha, amewataka watumishi wa TASAC kuendelea kushikamana na kuipa familia faraja na msaada unaohitajika.
Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi, shughuli za maombolezo zinaendelea nyumbani kwa marehemu, Changanyikeni, jijini Dar es Salaam. Kesho, Jumapili tarehe 2 Agosti 2026, kutafanyika ibada fupi, pamoja na kusomwa kwa wasifu wa marehemu, salamu za rambirambi na kuaga mwili.
Baada ya taratibu hizo, safari ya kuelekea Kibosho, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, itaanza kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika siku ya Jumatatu, tarehe 3 Agosti 2026.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.