MKURUGENZI MKUU TASAC ASHEREKEA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA NA WADAU
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, leo tarehe 07 Oktoba, 2026 ameshiriki katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja na Wadau kwa kuzungumza na makundi mbalimbali yanayohudumiwa na Shirika, wakiwemo mabaharia, wanafunzi na watumishi wa Chuo cha Mafunzo ya Bahari Dar es Salaam (DMTA), pamoja na watumishi wa TASAC.
Maadhimisho hayo yanafanyika sambamba na kaulimbiu ya mwaka huu, “The Extra Mile,” inayohimiza taasisi na watumishi kwenda hatua ya ziada katika kuhakikisha wateja na wadau wanapata huduma bora, kwa wakati na zinazozingatia mahitaji yao.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Bw. Salum amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha huduma zinazotolewa na TASAC, akieleza kuwa huduma bora ni msingi wa kujenga uaminifu, kuimarisha uhusiano na wadau na kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri majini.
Amesema TASAC imeanza kutumia mfumo mpya wa kielektroniki wa “Maritime Transport Regulatory System (MTRS)” unaolenga kurahisisha, kuharakisha na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za udhibiti katika sekta ya usafiri majini.
Ameongeza kuwa Shirika lipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuanza kutoa vyeti kidijitali, hatua itakayopunguza matumizi ya nyaraka za karatasi, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza uwazi na ufanisi.
Katika tukio hilo, Bw. Salum, ambaye pia ni Msajili wa Mabaharia nchini, ametumia nafasi hiyo kusajili mabaharia na kutoa vyeti kwa waliokidhi vigezo, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana kwa wakati na kwa ufanisi.
Akizungumza na mabaharia, Bw. Salum amesisitiza umuhimu wa kuboresha huduma zinazohusiana na usalama, ustawi na maendeleo yao, huku akiwataka kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia viwango vya usalama.
Kupitia kaulimbiu ya “The Extra Mile” TASAC inaendelea kuimarisha huduma kwa wateja na wadau kwa kutumia teknolojia, kuboresha mifumo na kuhakikisha mahitaji yao yanazingatiwa katika utekelezaji wa majukumu ya Shirika.