MKOA WA DODOMA WAIPONGEZA TASAC KWA KUUNGANISHA WADAU KUTATUA CHANGAMOTO ZA FOLENI NA KUIMARISHA SEKTA YA UCHUKUZI
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Janeth Mayanja, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, ameipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa juhudi za kuratibu na kuunganisha wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi katika kutafuta suluhisho la changamoto ya foleni ya magari ya mizigo, pamoja na kuboresha ufanisi wa usafirishaji wa shehena nchini.
Mhe. Mayanja ametoa pongezi hizo leo, tarehe 5 Novemba, 2026, alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wakati wa kikao na Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC iliyomtembelea ofisini kwake mkoani Dodoma.
Amesema Mkoa wa Dodoma una fursa kubwa ya kuwa kitovu muhimu cha shughuli za usafirishaji na biashara nchini, hususan kupitia uwekezaji katika miundombinu ya bandari kavu, ambayo itasaidia kupunguza msongamano wa magari ya mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam na kurahisisha mtiririko wa shehena kwenda maeneo mbalimbali ya nchi na nchi jirani.
Aidha, ameeleza kuwa Mkoa wa Dodoma una maeneo yenye fursa mbalimbali za uwekezaji na kutoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa hizo, huku akisisitiza kuwa Serikali ya Mkoa iko tayari kushirikiana nao kuwezesha uwekezaji wenye tija kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mayanja ameiomba TASAC kuwa balozi wa Mkoa wa Dodoma kwa kutangaza fursa zilizopo na kuhamasisha wawekezaji kuchangamkia uwekezaji katika sekta ya usafirishaji, hususan huduma na miundombinu ya bandari kavu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC, Nahodha Mussa Mandia, amesema ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi ya kufuatilia maendeleo ya miundombinu na shughuli za sekta ya uchukuzi, kujionea hali halisi ya utoaji huduma pamoja na kuimarisha ushirikiano na Serikali za Mikoa na wadau mbalimbali.
Ameeleza kuwa katika ziara hiyo mkoani Dodoma, Bodi imetembelea maeneo ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) yaliyopo Ihumwa na Bahi, yanayohusika na shughuli za kuhudumia na kusafirisha shehena za mizigo kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema ziara hiyo inalenga kutathmini hali ya miundombinu na shughuli za usafirishaji katika maeneo hayo, kubaini fursa za uwekezaji na maboresho, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati utakaosaidia kuongeza ufanisi wa huduma za usafirishaji na kupunguza changamoto zinazokwamisha mtiririko wa shehena nchini.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mfumo wa usafirishaji wa shehena nchini kwa kuunganisha wadau, kuboresha miundombinu na kutumia fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali ya nchi.