Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

BODI YA WAKURUGENZI TASAC YATEMBELEA MIUNDOMBINU YA BANDARI KAVU MOROGORO

Imewekwa: 05 November, 2026
BODI YA WAKURUGENZI TASAC YATEMBELEA MIUNDOMBINU YA BANDARI KAVU MOROGORO

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Nahodha Mussa Mandia, leo tarehe 4 Novemba, 2026, ameongoza wajumbe wa Bodi kutembelea Bandari Kavu ya Mkwawa na Kituo cha Kuhudumia Mizigo cha Reli (TRC ICD) mkoani Morogoro, kujionea maendeleo ya miundombinu na uwekezaji katika sekta ya usafirishaji.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Nahodha Mandia amesema uwekezaji katika miundombinu ya usafirishaji pamoja na ukuaji wa sekta ya viwanda mkoani Morogoro unafungua fursa kubwa za kukuza biashara na uwekezaji. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usafirishaji ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.

Amesema ni muhimu kuwekeza katika ujenzi wa barabara za nje ya mji (Ring Roads) pamoja na kuimarisha mifumo ya reli inayounganisha maeneo ya viwanda na vituo vya kuhudumia mizigo. Hatua hiyo itarahisisha usafirishaji wa malighafi na bidhaa, kupunguza gharama na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi.

Aidha, amesema kuwa Bodi ya Wakurugenzi TASAC itaendelea kuishauri Serikali kuhusu maendeleo ya miundombinu ya usafirishaji ili kuimarisha muunganiko wa mifumo ya reli na barabara na kuchochea ukuaji wa sekta hiyo nchini.

Katika ziara hiyo, wawekezaji, wafanyabiashara na wasafirishaji wa mizigo wameipongeza Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa uwekezaji katika Reli ya Kisasa (SGR), wakieleza kuwa mfumo huo una mchango mkubwa katika kuboresha usafirishaji wa mizigo, kupunguza muda wa safari na gharama za biashara. Pia wamehimiza kuendelea kuongeza uwezo wa huduma hizo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dkt. Mussa Ali Mussa, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza miundombinu ya reli ili kuimarisha huduma za usafirishaji na kukuza shughuli za kiuchumi mkoani humo.

Kwa upande wake, mwakilishi wa TRC, Bw. Rafael Bwire, amesema shirika hilo linaendelea kupanua na kuboresha miundombinu ya reli ili kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena na kukidhi mahitaji ya wadau.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Bodi ya TASAC kuimarisha ushirikiano na wadau katika kuboresha huduma za usafirishaji, kukuza biashara na kuwezesha uwekezaji nchini.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo