Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

MHE. NYONGO: PWANI NI LANG0 LA BIASHARA, KUENDELEA PUNGUZA FOLENI BANDARI YA DAR ES SALAAM

Imewekwa: 04 November, 2026
MHE. NYONGO: PWANI NI LANG0 LA BIASHARA, KUENDELEA PUNGUZA FOLENI BANDARI YA DAR ES SALAAM

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Nyongo, amesema Mkoa wa Pwani ni lango la biashara nchini Tanzania, na uko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa sekta ya usafirishaji na biashara katika kuwezesha kupunguza msongamano wa magari na foleni ya shehena katika Bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza leo, tarehe 3 Novemba 2026, na ugeni wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mhe. Nyongo amesema Mkoa wa Pwani una nafasi muhimu katika kukuza biashara na kurahisisha shughuli za usafirishaji kutokana na uwepo wa miundombinu na maeneo yenye fursa za uwekezaji.

Amesisitiza kuwa matumizi ya Bandari Kavu ya Kwala ni miongoni mwa mikakati muhimu inayoweza kusaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwezesha shughuli za upokeaji, uhifadhi na usambazaji wa shehena kufanyika kwa ufanisi zaidi.

Aidha, amesema Mkoa wa Pwani uko tayari kutoa ushirikiano unaohitajika, kupokea ushauri na kuendelea kushirikiana na TASAC pamoja na wadau wengine katika kuboresha huduma za usafirishaji na biashara. Ameeleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuhakikisha miundombinu iliyopo inatumika kikamilifu kwa manufaa ya uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC, Nahodha Mussa Mandia, amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukagua miundombinu ya bandari kavu zilizopo katika Mkoa wa Pwani ili kujionea hali ya miundombinu, uwezo wake wa kuhudumia shehena pamoja na mchango wake katika kurahisisha shughuli za usafirishaji na biashara.

Amesema ziara hiyo pia inalenga kutathmini fursa zilizopo katika bandari hizo, hususan Bandari Kavu ya Kwala, katika kusaidia kupunguza msongamano wa shehena na magari katika Bandari ya Dar es Salaam, kuongeza ufanisi wa huduma za bandari na kuimarisha mfumo wa usafirishaji wa mizigo nchini.

Katika ziara hiyo, Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC pia walitembelea eneo la Kongani ya Viwanda ya Kwala pamoja na Kituo cha Upangaji na Uunganishaji wa Treni cha Ruvu (Ruvu Marshalling).

Mrejesho, Malalamiko au Wazo