Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

DG TASAC: BANDARI KAVU ZAONGEZA UFANISI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM

Imewekwa: 01 September, 2026
DG TASAC: BANDARI KAVU ZAONGEZA UFANISI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, amesema uanzishwaji na uendeshaji wa bandari kavu umechangia kupunguza msongamano wa shehena na kuongeza ufanisi zaidi wa Bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza Agosti 31, 2026, katika Ukumbi wa PSSSF Dar es Salaam, Bw. Salum amesema ongezeko la shehena limeongeza mahitaji ya maeneo mbadala ya kuhifadhi na kuhudumia makasha.

Amesema kati ya mwaka 2021 na 2025, shehena iliyohudumiwa bandarini iliongezeka kwa asilimia 88, kutoka tani milioni 16.9 hadi milioni 31.8, huku shehena ya makasha ikiongezeka kwa asilimia 58, kutoka makasha 749,850 hadi 1,185,153.

“Bandari kavu husaidia kupunguza msongamano bandarini na kuiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kutoa huduma kwa ufanisi zaidi. Bandari hii ni kitovu cha uchumi wa Taifa na biashara ya kikanda,” amesema Bw. Salum.

Amesema Bandari ya Dar es Salaam ina uwezo wa kuhifadhi makasha 27,900. Julai 2026, eneo la bandari linaloendeshwa na TEAGTL lilihudumia makasha 91,625, hali inayoonesha ongezeko la mizigo.

Bw. Salum amesema Serikali imeendelea kuongeza uwezo wa kuhudumia mizigo kwa kuanzisha bandari kavu Kwala, Morogoro na Isaka, pamoja na kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi katika miundombinu ya usafirishaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Abed Galius, amesema TPA inaendelea kuboresha uwezo wa kuhifadhi na kuhamisha makontena ili kukabiliana na ongezeko la mizigo na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara kikanda.

Aidha, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Bandari Kavu, Bw. Meleck Shange, amesema sekta binafsi ina wajibu wa kuwekeza katika bandari kavu, vifaa, mifumo na nguvu kazi, huku Serikali ikisimamia usalama wa huduma.

TASAC inaendelea kuimarisha usimamizi wa bandari kavu kwa kuhakikisha zina maeneo na maegesho ya kutosha, barabara zenye uwezo unaothibitishwa na TARURA au TANROADS, na ujazo wa mizigo usiozidi asilimia 60. Na kwa sasa TASAC pia imesitisha kwa muda utoaji wa leseni mpya za bandari kavu Dar es Salaam.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo