Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

DC MULEBA AIPONGEZA TASAC KUIMARISHA USALAMA WA USAFIRI MAJINI

Imewekwa: 16 April, 2026
DC MULEBA AIPONGEZA TASAC KUIMARISHA USALAMA WA USAFIRI MAJINI

Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Abel Nyamahanga, amelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa juhudi zake za udhibiti na usimamizi wa sekta ya usafiri kwa njia ya maji nchini hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali, hususan katika Wilaya ya Muleba. 

Mhe. Nyamahanga amebainisha hayo alipokua  anazungumza na wataalamu kutoka TASAC na Shirika la Bima la Taifa (NIC) waliomtembelea ofisini kwake,  tarehe 13 Aprili, 2026,

Ameongeza kuwa hatua hizo zimeongeza imani ya wananchi katika usafiri wa majini na kuimarisha usalama wa abiria.

Mhe. Nyamahanga amesisitiza umuhimu wa ukusanyaji sahihi wa taarifa za mizigo na abiria kwenye “manifest”, akionya dhidi ya udanganyifu unaoweza kuhatarisha maisha ya watu na kuchelewesha huduma za uokoaji pindi majanga yanapotokea.

Ameeleza kuwa taarifa sahihi ni nyenzo muhimu katika kurahisisha operesheni za uokoaji na pia kusaidia kampuni za bima kulipa fidia kwa haraka kwa kuzingatia nyaraka halali bila usumbufu wowote.

Katika hatua nyingine, Nyamahanga ameziagiza TASAC na NIC kuendelea kutoa elimu ya usalama na bima kwa wadau wote wa sekta ya usafiri majini, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria za upakiaji. Alikataza vitendo vya kuchanganya mizigo na abiria au kusafirisha watu pamoja na mifugo ndani ya chombo kimoja bila kufuata taratibu, akieleza kuwa hali hiyo ni hatari na inachangia ajali zisizo za lazima.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Kagera, Nahodha Mzee Mvihanga, amesema kuwa TASAC kwa kushirikiana na NIC wanaendelea kutoa elimu ya usafiri salama na masuala ya bima ili kuhakikisha usafiri kwa njia ya maji unaimarishwa.

Kwa upande wake, Afisa Bima wa NIC Mkoa wa Kagera, Bw. Alfred Bwojo, amebainisha kuwa sekta ya usafiri majini inakabiliwa na hatari mbalimbali, hivyo ni muhimu kwa wamiliki wa vyombo, wasafirishaji na wafanyabiashara kuchangamkia huduma za bima ili kujihakikishia ulinzi wakati wote wa safari.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo