Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

WAZIRI MKUU AZITAKA TAASISI ZA UCHUKUZI KUONGEZA UWAJIBIKAJI NA KULINDA UWEKEZAJI WA MIUNDOMBINU

Imewekwa: 16 November, 2026
WAZIRI MKUU AZITAKA TAASISI ZA UCHUKUZI KUONGEZA UWAJIBIKAJI NA KULINDA UWEKEZAJI WA MIUNDOMBINU

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amezitaka taasisi za sekta ya uchukuzi nchini, ikiwemo Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), kuongeza uwajibikaji, kuimarisha usimamizi wa miundombinu na kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unatoa huduma bora na manufaa ya muda mrefu kwa wananchi.

Ameyasema hayo leo, tarehe 16 Novemba 2026, wakati akifungua Mkutano wa 19 wa Wadau wa Sekta ya Uchukuzi na Tathmini ya Utendaji Kazi wa Sekta hiyo, uliofanyika katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza.

Amesema Serikali imewekeza mabilioni ya shilingi katika ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa, hivyo ni muhimu kuhakikisha vinatunzwa ili kuepusha gharama za ziada zinazotokana na uharibifu unaoweza kuzuilika.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama, ubora wa huduma, matengenezo endelevu ya miundombinu, matumizi ya teknolojia za kidijitali na ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuongeza ufanisi na ushindani wa kiuchumi.

Kwa upande wa usafiri wa majini, maelekezo hayo yanaendana na jukumu la TASAC la kusimamia usalama wa vyombo vya majini, kulinda mazingira ya majini na kuhakikisha huduma zinazingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.

Waziri Mkuu amesema miundombinu bora ya uchukuzi ni msingi wa kukuza biashara za ndani, kikanda na kimataifa, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha muunganiko wa usafiri na nchi jirani ili kupanua fursa za biashara.

“Kuruhusu miundombinu iharibike ni kurudia kutumia mabilioni ya fedha ambayo tayari yamekwishawekezwa. Tunapaswa kuimarisha matengenezo endelevu, usalama na ubora wa huduma,” amesema Dkt. Nchemba.

Vilevile, amezitaka taasisi za sekta hiyo kuimarisha upimaji wa utendaji kazi, uwazi katika utoaji wa huduma na nidhamu ya matumizi ya fedha ili kuhakikisha uwekezaji unaleta manufaa kwa wananchi.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi na watendaji kutoka Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi, taasisi zilizo chini ya wizara hizo, wadau pamoja na washirika wa maendeleo.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo